Header Ads Widget

VIONGOZI VYAMA VYA SIASA KUJENGEWA UWEZO KUHUSU MAADAILI,ULINZI WA DATA NA UWAJIBIKAJI.

 

Na matukio Daima App.

DAR ES SALAAM:

 MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema wameanza kutekeleza programu ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maadili, ulinzi wa data na uwajibikaji katika kipindi cha uchaguzi.

Akifungua kikao kazi kati ya ofisi hiyo na wahariri wa vyombo vya habari leo Mei 3, 2025 jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi amesema programu hiyo imeanza kutekelezwa Zanzibar na wiki ijayo itafanyika Dar es Salaam lengo kuhakikisha wanakuwa na maarifa sahihi ya uchaguzi kwa njia ya amani na utawala wa kisheria.

Amesema wanashirikiana na wadau wengine wa uchaguzi ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), vyombo vya habari na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuhakikisha vyama vya siasa vinapata uelewa.

Ameeleza ushirikiano huo unalenga kuwa na uchaguzi huru, haki na wenye amani na kwamba vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee kuhakikisha uchaguzi wa amani hivyo aliwataka kuripoti habari zilizosahihi, za haki na zisizoegemea upande wowote.

"Tuna mpango wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu sheria tunazozisimamia, kuwezesha kuwa na uchaguzi wa kidemokrasia na maadili," amesema Jaji Mutungi.

Msajili huyo pia amefafanua watahakikisha vijana na wanawake wanapata fursa sawa za kushiriki katika uchaguzi huo kwa kupiga kura, kugombea nafasi za uongozi na kushiriki katika midahalo.

Kuhusu suala hilo, ameeleza vyombo vya habari vinaweza kuwa daraja la kukuza uelewa, kuondoa hofu na kutoa jukwaa la kujieleza kwa makundi hayo na kupendekeza mashirika ya habari yashirikiane na ofisi hiyo katika kampeni za kuhamasisha ushiriki wa makundi hayo.

Katika hatua nyingine, Jaji Mutungi amewatahadharisha waandishi wa habari nchini kuhakikisha wanapata habari za siasa kwenye vyanzo vya kuaminika, kuepuka taharuki na usambazaji wa habari za uongo.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI