Header Ads Widget

VIJANA WA UDOM WAPATIWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KUPITIA SANAA



   Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

Zaidi ya vijana 150 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walishiriki katika warsha ya ujasiriamali inayolenga kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia sanaa.  Warsha hii ilifadhiliwa na Universal Music Group East Africa na kuendeshwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF), Mkeka na Kanga Foundation, na Ruge Mutahaba Foundation. 

Vanessa Anyoti, Mkurugenzi Mtendaji wa JMKF, alieleza kuwa warsha hii inatekeleza dhamira ya taasisi hiyo ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa karne ya 21 unaowawezesha kuunda na kupata fursa za ajira zenye maana.  Alisema, "Uamuzi wetu wa kukuza vipaji vya vijana katika sanaa na kukuza ajira unalingana kikamilifu na dhamira ya taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete ya kuwezesha vijana kupata ujuzi wa karne ambao unawezesha kuunda na kupata fursa za ajira zenye maana." 


Mbunifu wa vitu asili kutoka Taasisi ya AYMA alieleza kuwa wameanza kutoa mafunzo katika chuo cha Dodoma UDOM kwa sababu chuo hicho kinamasomo ya sanaa, lakini wanampango wa kwenda kwenye vyuo vingi zaidi ili kuwaonyesha vijana jinsi wanavyoweza kutengeneza ajira zao kwa kutumia sanaa na utalii.  Alisema, "Tupo tunaishi kwenye jamii ambayo vijana ni vigumu kupata ajira, hivyo mpango huu utakwenda kuwachechemua kufikiri kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa. Kupitia sanaa wataweza kujiajiri na kuhudumia familia zao." 

Mkeka na Kanga Foundation haijaanza hivi karibuni, kwani huwa wanapata wasaa wa kuzungumza na watoto wadogo kwa sababu wanaamini kipaji kinaanzia kwa mtoto.  Pia wanamipango ya kuwafikia vijana wote waliopo shule, vyuoni, na hata mitaani ili kuwafundisha masuala ya sanaa na sanaa.  Alisema, "Wito wangu kwa vijana ni kujihusisha sana kwa kuwa na vikundi kufanya kazi kwa pamoja; itakuwa rahisi kufikiwa." 


Faith Nzaro, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika masomo ya International Relations, alisema, "Nimejifunza vitu vingi hasa katika masuala ya ujasiriamali. Sasa naweza kujua ni namna gani nitakavyoweza kujiajiri mwenyewe baada ya kumaliza shule." 

Kelvin Kissato, mwanafunzi wa Social Humanities, alisema, "Kabla ya kuja katika mafunzo haya, nilikuwa na ndoto ya kuwa mjasiriamali, lakini nilikuwa sijui ni biashara gani nianze. Sasa na uelewa zaidi." 

Viongozi wa taasisi hizi wamehimiza taasisi nyingine zinazojihusisha na uhamasishaji wa vijana kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizi, ili kuwasaidia vijana wengi zaidi katika kujiajiri na kukuza vipaji vyao. 

Kwa ujumla, ushirikiano huu unalenga kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuwapa vijana zana na ujuzi wa kujitegemea kupitia sanaa na ujasiriamali. 




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI