NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mufindi, Jasmine Ng'umbi, ametoa wito kwa vijana kote nchini, hususan wale wa Wilaya ya Mufindi, kuchangamkia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri kupitia mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza na Matukio Daima Media, Jasmine alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha hizi kwa lengo la kuwawezesha vijana na makundi mengine maalum kuboresha maisha yao kupitia miradi ya kiuchumi.
Jasmine alisema kuwa vijana wengi bado hawajatambua uzito na fursa iliyopo katika mikopo hii ya Halmashauri, ambayo tofauti na mikopo mingine ya kibiashara, haina riba na imekusudiwa kuwasaidia vijana kuinuka kiuchumi.
Alisema kuwa ni muhimu kwa vijana kujitokeza kwa wingi kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ambavyo vinasajiliwa rasmi ili waweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Jasmine alisema badala ya vijana kukimbilia mikopo ya kibiashara kutoka taasisi binafsi ambazo zina masharti magumu na viwango vikubwa vya riba, ni busara zaidi kuchangamkia mikopo inayotolewa na serikali ambayo ni nafuu na inalenga kuboresha maisha ya wananchi.
Kuwa serikali ya awamu ya sita imeonyesha nia ya dhati ya kuwekeza kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kutenga asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya makundi haya.
“Tuishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya makundi haya ni jambo jema na linastahili pongezi kubwa sana kwa sababu linaonesha namna serikali ilivyojikita katika kuinua maisha ya wananchi wake, hususan vijana,” alisema Jasmine.
Alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya vijana ni ukosefu wa uelewa juu ya namna ya kuunda vikundi vya kiuchumi pamoja na kuandika maandiko ya miradi ya maendeleo.
Kuwa changamoto hiyo imekuwa kikwazo kwa vijana wengi kushindwa kunufaika na mikopo hiyo licha ya serikali kuweka mazingira bora ya upatikanaji wake.
Hivyo Jasmine aliwahimiza vijana kutambua kuwa kila kata ina maofisa maendeleo ya jamii ambao kazi yao ni kusaidia jamii katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia miradi ya maendeleo.
Alisema maofisa hao wanalipwa mishahara na serikali kwa ajili ya kusaidia wananchi, hivyo vijana wanapaswa kuwafuata na kuomba msaada wa kitaalamu ili waweze kufanikisha maandiko ya miradi na kuunda vikundi vinavyokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo.
“Hao maofisa maendeleo ya jamii wapo kwenye kata zetu wanalipwa kwa ajili ya kutusaidia sisi wananchi Vijana msisite kuwaendea, waombeni msaada wa kuandaa maandiko ya miradi, kuunda vikundi, na kuelekezwa namna ya kuomba mikopo ya Halmashauri,” alisema Jasmine.
Pia alitoa rai kwa vijana wote wa UVCCM kuendelea kuwa mabalozi wa elimu ya mikopo hiyo katika maeneo yao kwa kuwahamasisha vijana wengine ambao bado hawajajiunga katika vikundi au hawajui uwepo wa fursa hizo.
Alisema elimu ikisambazwa kwa njia ya maelezo ya ana kwa ana, mikutano, semina na hata mitandao ya kijamii, inaweza kuwafikia vijana wengi na hivyo kuongeza idadi ya walionufaika na mikopo ya serikali.
Jasmine Ng'umbi alisema iwapo vijana watachukua hatua na kuchangamkia mikopo hiyo, wataweza kujikwamua kiuchumi, kupunguza utegemezi, kuongeza ajira na hatimaye kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa, na iwapo watawezeshwa ipasavyo, taifa litakuwa na uhakika wa mafanikio ya kiuchumi na kijamii katika siku za usoni.
“Ni jukumu letu vijana kuona umuhimu wa kujituma na kutumia kila fursa ambayo serikali yetu inaitoa tuachane na fikra za kusubiri au kulalamika hebu tusimame kwa pamoja, tujiunge vikundi, tuandike miradi na tukatekeleze kwani hii ni fursa ya kipekee kwa kizazi chetu,” alihitimisha.
0 Comments