Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitia Wilaya ya Iringa Mjini, Islam Huwel, amewataka wana CCM na Watanzania kwa ujumla wasikate tamaa wala kuwa na hofu ya kusimama hadharani kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika kipindi cha Tanzania ya Leo kupitia Matukio Daima Media, Huwel alisema kuwa ni wakati wa kila mmoja kutembea kifua mbele na kueleza kwa uwazi kazi nzuri zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita.
Kuwa watanzania wengi ni mashuhuda wa mafanikio hayo, hivyo hakuna sababu ya kuwa kimya au kutembea kinyonge kana kwamba hakuna kinachoendelea.
“Kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia, hakuna sababu ya kutembea kinyonge kila mmoja anatakiwa kutembea kifua mbele na kujivunia maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa kote nchini,” alisema Huwel kwa msisitizo.
Huwel alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu, nishati na maji, ambayo yote ni mafanikio yanayoonekana kwa macho na kuguswa moja kwa moja na maisha ya wananchi wa kawaida.
Kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa kiongozi mwenye maono makubwa na msimamo wa kuhakikisha nchi inasonga mbele kwa kasi, huku akihimiza mshikamano, upendo na maelewano miongoni mwa Watanzania.
Hata hivyo alisema Rais amekuwa akisimamia vizuri misingi ya haki, demokrasia, na uwajibikaji serikalini.
Aliwataka wana CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa mabalozi wa kueleza mafanikio ya serikali, hasa katika ngazi za jamii, kwa kuwa kuna baadhi ya watu ambao bado hawana uelewa wa kina juu ya kazi nzuri zinazofanywa na serikali.
“Kwa nafasi yangu ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, pamoja na viongozi wenzangu, hatutakaa kimya. Tutaendelea kupongeza jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na kuhakikisha tunazieleza kwa wananchi wote, ili wale wachache ambao bado hawajafikiwa na taarifa hizi waweze kufahamu,” aliongeza Huwel.
Alisema Watanzania hawapaswi kuchoka kuisemea serikali yao na kuitetea inapofanya mambo mazuri kwa kuwa huo ni uzalendo.
kuwa mara nyingi wapinzani au watu wanaopinga maendeleo hawakosi cha kusema, hivyo ni muhimu wanaoona mema wasibaki kimya.
“Ni muhimu kusimama imara na kusema ukweli hili ni suala la uzalendo tusimame kifua mbele kusema kazi zinazofanywa na Rais wetu na tusiwaachie watu wachache wenye lengo la kupotosha jamii,” alisema Huwel.
Alisema kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kufanikishwa kwa kelele au maneno ya kupinga kila jambo, bali kwa vitendo vya ushirikiano na kuthamini jitihada za viongozi walioko madarakani.
Akitolea mfano wa miradi ujenzi wa shule na vituo vya afya, barabara na madaraja inayotekelezwa kila kona ya nchi kuwa ni ushahidi tosha wa serikali yenye dira.
Aliwataka vijana, wanawake, wazee na makundi yote ya jamii kuwa sehemu ya safu ya kuhamasisha maendeleo na si kuwa watazamaji au wakosoaji bila hoja.
Kuwa ni wakati wa kila Mtanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kushikamana, kufanya kazi kwa bidii na kutambua mchango wa viongozi wetu katika maendeleo.
Rais Samia anaonyesha ujasiri, uadilifu na hekima ya hali ya juu katika kuiongoza nchi, huku akihimiza usawa wa kijinsia, maendeleo jumuishi na uwazi wa matumizi ya rasilimali za umma.
Katika hitimisho lake, Huwel alitoa rai kwa viongozi wa chama, mashina ya CCM, na wanachama wa kawaida kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kutoa elimu ya maendeleo na kueleza kwa kina kazi nzuri zinazotekelezwa na serikali ya CCM, kwa kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kuhakikisha chama kinaendelea kuwa karibu na wananchi.
“Tusimame kifua mbele tuseme, tufafanue, tuelimishe tusiache watu waongee uongo huku sisi wenye ukweli tukinyamaza Serikali inafanya kazi. Rais Dkt. Samia ni kiongozi makini na mzalendo wa kweli. Kila Mtanzania anapaswa kujivunia hilo,” alihitimisha Huwel.
0 Comments