Header Ads Widget

UNYWAJI POMBE KUPITILIZA MAUMIVU KWA WATOTO

NA RACHEL  MRISHO,MATUKIO DAIMA MEDIA

MALEZI ni msingi mkubwa katika kumjenga mtoto kwa mustakabali wa maisha yake.

Kwa kawaida ukuaji wa mtoto huendana na jinsi wazazi wanavyotaka. Ni rahisi sana mtoto kuiga mienendo ya wazazi wake, mfano kama wazazi ni wacha Mungu mtoto anaweza kufuata nyendo hizo, halikadhalika kama mzazi ni mlevi mtoto anaweza kuiga tabia hiyo.

Makala haya nitazungumzia ulevi wa kupitiliza kwa wazazi unavyoathiri malezi na makuzi ya watoto.

Ingawa ulevi huathiri zaidi anayetumia lakini pia una madhara makubwa kwa familia na jamii kwa ujumla.

Athari za ulevi wa wazazi kwa watoto ni kubwa zaidi na mara nyingi huwa hazionekani wazi, athari hizo zinapokuja kujitokeza huharibu maisha ya watoto.

Baadhi ya wazazi huwanywesha pombe watoto wadogo wakiwamo wachanga hususan wanaoshumbuliwa na tumbo wakidai kuwa pombe ni dawa ya tumbo, kama hiyo haitoshi wengine huwapa watoto wanaosumbua kulala. 

Kiafya athari zipo athari nyingi  za kuwapa watoto pombe ikiwamo magonjwa ya figo, ini pia hudumaza ukuaji wa mtoto.

Umri ambao watoto hupewa pombe hadharani ni kuanzia miaka mitatu na kuendelea, wazazi hufanya hivyo wakifurahia mtoto anavyoyumba ama kufanya vituko huku wao wakifurahia.

Mtoto anayeanzishwa pombe akiwa na umri huo ni wazi kuwa maisha yake yanaharibiwa na wazazi wake, kwa minajili hiyo mtoto huyo akiendelea kunywa pombe ni vigumu kumuondoa kwenye kundi la walevi anapokuwa kijana.

Ukiacha madhara hayo ulevi wa wazazi kwa ujumla husababisha matatizo ya afya ya akili kwa watoto, wasiwasi, huzuni na wakati mwingine huchangia tabia mbaya ikiwamo uhalifu na ukosefu wa maadili.

Mzazi mlevi huwa tishio kwa watoto, ni rahisi kuanzisha ugomvi, kutoa lugha chafu na wakati mwingine kupigana hadharani.

Matendo hayo huwajengea watoto hofu, ukatili na pia huchangia kuweka matabaka kati ya wazazi wao hasa inapotokea mzazi mmoja kuwa mlevi wa kupindukia, watoto hujenga chuki naye.

Matatizo ya afya ya akili kwa watoto huchangiwa na hali   ya wasiwasi, hasa wanapomshuhudia mzazi kufanya mambo ya ovyo mbele yao kutokana na ulevi.

Aidha, changamoto hiyo ya ulevi huwasababishia watoto kuwa na huzuni, hawafurahii maisha wao na wazazi wao pia, hawapati muda wa kusikilizwa shida zao.

Ifahamike kuwa wajibu wa wazazi ni kuwalinda watoto wasijihusishe na vitendo viovu ikiwamo matumizi ya pombe wakiwa wadogo. Pia, ni dhana potovu kufikiri kuwa pombe inatibu matatizo ya tumbo kwa watoto.

Si jambo zuri wazazi kunywa pombe kupitiliza tabia hiyo inawapa adhabu kali watoto.

Ni muhimu wazazi wazingatia matangazo yanayotolewa kuwa watoto chini ya miaka 18 wasitumie vileo.

Kwa maoni na ushauri piga Simu namba 0747 604000/0754026299 


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI