Na Farida Mangube, Morogoro
Katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeahidi kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wake.
Akizungumza kwenye hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya wafanyakazi wa SUA mara baada ya maadhimisho hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala, Amandus Muhairwa, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, alisema menejimenti ya SUA inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi.
“Tunatambua mchango wa wafanyakazi na juhudi za viongozi wa vyama vya wafanyakazi chuoni hapa. Pia nawapongeza waliopata tuzo za utendaji bora,” alisema Muhairwa, huku akiwahimiza wafanyakazi kujitokeza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 2025.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa RAAWU tawi la SUA, Bw. Faraja Kamendu, akisoma risala ya wafanyakazi, aliushukuru uongozi wa Chuo kwa ushirikiano mzuri na kuwasihi wafanyakazi kutimiza wajibu wao huku wakidumisha upendo wenye tija na kusimamia nguzo ya umoja bila matabaka, akisisitiza kuwa mshikamano ni msingi wa mafanikio.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi THTU tawi la SUA, Dkt. Nickson Mkiramweni, aliwahimiza wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaleta manufaa makubwa katika kupigania haki na usawa mahali pa kazi.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kwa mwaka 2025 yamebebwa na kaulimbiu isemayo: “Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi – Sote Tushiriki.”
0 Comments