Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, ameibua hisia nzito kwa kulaani vikali tabia ya baadhi ya vijana kutoka Kenya waliotumia mitandao ya kijamii kutoa matusi na kejeli dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema hatua hiyo ni fedheha kwa heshima ya viongozi wa Afrika na ni kinyume na maadili ya Kiafrika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Dodoma Sheikh Alhad alisema kitendo hicho hakipaswi kuvumiliwa na kinapaswa kukemewa na watu wa mataifa yote yenye kuthamini maadili, heshima na utu wa binadamu.
“Kumshambulia Rais wa nchi kwa matusi si uhuru wa kujieleza bali ni upungufu wa maadili. Samia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama wa Taifa. Huwezi kumpa kejeli au kumshusha heshima yake hadharani, halafu tukaitazama tu. Hili tunalikemea kwa nguvu zote,” alisema Sheikh Alhad kwa msisitizo.
Amesema kuwa tabia ya kudhalilisha viongozi wa kitaifa ni sumu ya utulivu na hujenga chuki zisizokuwa na msingi kati ya mataifa na jamii. Ameongeza kuwa lugha za kejeli na matusi mitandaoni zimekuwa zikitumiwa vibaya na baadhi ya watu wasio na maadili, hali inayohatarisha ustaarabu wa bara la Afrika.“
Tanzania na Kenya ni mataifa yenye historia ya undugu, lakini matendo ya vijana wachache yasiwe chanzo cha kuvuruga uhusiano wetu. Ni wajibu wa kila mmoja kulinda heshima ya viongozi wa Afrika bila kujali taifa lake. Na sisi tunasema kwa sauti — Rais wetu hatakiwi kutukanwa,” alisema.
Aidha, Sheikh Alhad aliwahimiza vijana wa Tanzania kujitofautisha na mtindo huo mbovu kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa ujenzi wa taifa, ujasiriamali, elimu na maadili, badala ya kutumiwa kueneza chuki na udhalilishaji.“
Vijana wetu ni nguzo ya taifa. Tuwafundishe kusema ukweli kwa staha, kutoa maoni kwa heshima, na kutetea haki kwa hoja, si kwa matusi,” aliongeza.
Katika kuendeleza juhudi hizo, JMAT imepanga kuzindua kampeni ya kitaifa itakayolenga kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya mitandao, pamoja na kulinda maadili na utu wa viongozi wote – hasa wanawake – dhidi ya matusi ya kingono, kejeli na propaganda za uchochezi.
Sheikh Alhad alihitimisha kwa kutoa wito kwa taasisi za sheria na udhibiti wa maudhui, pamoja na viongozi wa dini Afrika Mashariki, kushirikiana kukomesha tabia hiyo na kulinda heshima ya uongozi barani Afrika.
0 Comments