📌Wananchi wapewa elimu matumizi bora ya nishati ya umeme
📌Wahimizwa kujiunganisha na huduma ya umeme
📌Wananchi wahamasika na UMEME TAYARI ( Ready Board)
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuhamasisha matumizi sahihi na endelevu ya umeme kwa Watanzania ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi bora ya nishati, kuhamasisha kuunganisha umeme, tahadhari za umeme pamoja na utunzaji wa miundombinu ya umeme.
Hayo yamebainishwa na Wataalam wa REA, TANESCO na Mkandarasi waliofika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kutumia fursa ya miradi ya REA inayotekelezwa mkoani Morogoro.
Akizungumza katika mkutano na wananchi, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Abdulrazack Mkomi amesema kuwa, lengo na dhamira ya serikali ni kuona mabadiliko yanatokea katika maeneo ya vijijini hasa kwenye nyanja za kiuchumi kama kuongezeka kwa fursa za ajira na viwanda vidogo vidogo, kuboresha sekta ya afya, sekta ya elimu na huduma zote muhimu za kijamii kwa ujumla.
Katika kunifanikisha hilo serikali kupitia wakala wa Nishati vijijini umeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini ikiwemo usambazaji wa nishati ya umeme ili nishati hiyo itumike kama silaha ya kuleta mabadiliko Vijijini.
Ameongeza kuwa, ili kuhamasisha matumizi bora ya nishati ya umeme, REA itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa kupita kaya kwa kaya , kitongoji kwa kitongoji , kijiji kwa kijiji ili kila mwanachi aweze kutumia nishati ya umeme vizuri na kujiletea maendeleo.
Naye, mtaalam kutoka kwa mkandarasi STEG INTERNATIONAL SERVICE , Mhandisi Fidoline Haule amesema kuwa REA pamoja na Mkandarasi wameendelea na uhamasishaji wananchi kuunganisha umeme kwenye vijiji na vitongoji mkoa wa Morogoro ili wananchi wachangamkie fursa hii wakati mkandarasi wa mradi akiwa bado yupo eneo la mradi ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya mradi kukamilika na kukabidhiwa TANESCO ikiwemo kubadilika kwa gharama za uunganishaji umeme.
Mkomi ameongeza kuwa, Serikali imeweka mkazo katika kusambaza umeme kwa watanzania ili kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kujenga uchumi imara na kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu kwa watanzania wote.
0 Comments