Na Shemsa Mussa -Matukio daima Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, amewasihi wananchi wa Mkoa wa Kagera na Mikoa ya jirani kuchangamkia fursa ya huduma za matibabu zitakazotolewa na Madaktari Bingwa na Ubingwa Bobeza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera itakayoanza tarehe 05.05.2025 hadi 09.05.2025.
Amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ngara.
RC Mwassa amesema kuwa, timu hiyo kubwa ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi watakuwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Hospitali zote za Rufaa za Mikoa zinazopatikana Kanda ya ziwa, Hospitali ya Kanda ya Bugando na Chato pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Amesistiza kuwa, lengo kuu la kambi hiyo ni kuwasaidia wananchi kupunguzia gharama za kusafiri kufuata matibabu kwenye hospitali kubwa zilizopo Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.
“Rais wetu ametambua changamoto za wananchi, hasa wale wasio na uwezo wa kusafiri kutafuta matibabu. Hii ni fursa ya kipekee. Ikiwa unaumwa au una mtoto anayehitaji matibabu, njoo upate huduma bora karibu na nyumbani, amesema Mhe, Mwassa"
Sambamba na hilo amesema kuwa, huduma za kibingwa zitakazotolewa ni pamoja na matibabu ya magonjwa ya upasuaji, magonjwa ya wanawake, magonjwa ya akili, magonjwa ya ndani, ini, figo, pua, koo, mfumo wa fahamu, mfumo wa mkojo, pamoja na huduma za mazoezi ya viungo na utengamano. Madaktari waliobobea katika kila eneo watakuwepo kutoa huduma hizo kwa ufanisi.
Ameongeza kuwa, huduma zitatolewa kwa wananchi kutoka wilaya zote za Kagera, mikoa jirani kama Kigoma na Geita, pamoja na nchi jirani zinazopakana na mkoa huo.
Amebainisha kuwa, wagonjwa wenye BIMA za afya watatumia BIMA zao kupata huduma, huku wale wasio na BIMA wataingizwa katika utaratibu wa kawaida wa hospitali wa kuchangia gharama za Afya.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Mseleta Nyakiroto, amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya kupokea madaktari hao mpaka sasa yamekamilika.
0 Comments