NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini, Afrey Nsomba, amewataka wanachama wa chama hicho kuendeleza mshikamano na ushirikiano wanapoelekea katika kipindi cha uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kuacha tofauti zao kwa maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya chama katika kata mbalimbali za jiji hilo, Nsomba amesema ni wakati wa wanachama kuweka mbele umoja na nidhamu ya chama, hasa katika kipindi hiki cha maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu.
“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha tunalinda heshima ya chama chetu kwa kushirikiana na kushikamana. Tofauti ndogondogo zisiturudishe nyuma,” alisema Nsomba.
Ziara hiyo imehusisha kata mbalimbali ambapo Mwenyekiti huyo alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa matawi, wajumbe wa mashina na wanachama kwa ujumla kuhusu hali ya chama na mikakati ya ushindi katika uchaguzi ujao.
Akiwa katika kata hizo, Nsomba pia alipongeza juhudi za wanachama na viongozi wa mitaa katika kuhakikisha shughuli za chama zinaendelea kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamasisha ushiriki wa vijana na wanawake katika shughuli za kisiasa.
0 Comments