NA MATUKIO DAIMA APP.
DAR ES SALAAM.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, imethibitisha kukamilika kwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo itazinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 17 Julai 2025 jijini Dodoma.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Prof. Kitila Mkumbo amesema dira hiyo ya miaka 25 imeandaliwa kwa ushirikishwaji mpana wa wananchi, taasisi, vyama vya siasa na wadau wa maendeleo.
Ameongeza kuwa dira hiyo inaweka msingi wa kujenga uchumi wa kati wa juu unaotegemea maarifa, teknolojia na usimamizi thabiti wa rasilimali za Taifa.
Katika mjadala huo, Idda Mushi, mmoja wa wanachama wa Jukwaa la Wahariri (TEF), alihoji iwapo kuna utaratibu wowote wa kuwawajibisha viongozi au Serikali zitakazokuja endapo zitapuuza au kwenda kinyume na Utekelezaji wa dira hiyo, ingawa Waziri Mkumbo Alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa kwenye hili kwa kuangalia iwapo bajeti zinazopendekezwa zinahusisha dira pamoja na kupata Utekelezaji kutoka kwa viongozi na wabunge.
Aidha Idda katika kikao hicho akapendekeza kwakuwa mabadiliko ya kiuchumi duniani yanaathiri dira za ndani, ni vyema msingi ya dira hiyo ikajengwa kwa kutegemea rasilimali Kuu za Ndani ya nchi ambazo haziwezi kutetereka kwa urahisi ikiwemo Dhahabu, gesi na nguvu kazi ya Vijana,
Idda pia akashauri umuhimu wa kuwa na msingi wa kisheria kwa utekelezaji wa dira hiyo ili kuhakikisha bajeti za kila mwaka zinaendana na malengo yaliyoainishwa.
Kuhusu rasilimali Kuu za Ndani, Waziri Mkumbo alisema mambo hayo yamezingatiwa Katika dira kwani tofauti ya Tanzania na nchi zingine,uchumi hautegemei chanzo kimoja bali mazao na bidhaa nyingi tegemeo kama zilizotajwa na nyingine nyingi ikiwemo utalii,viwanda na Kilimo na ndio maana uchumi wake ni stahimilivu na imara.
Waziri huyo pia aliunga mkono kuwa licha ya dira hiyo kuidhinishwa na Bunge, bado kuna haja ya kutungwa kwa sheria mahsusi ya utekelezaji wake kama walivyoshauri wahariri wengi waliokuwepo.
Prof. Kitila pia amevitaka vyama vya siasa kuifanya dira hiyo kuwa sehemu ya Ilani zao, akibainisha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tayari kimeianza hatua hiyo.
Kwa upande mwingine, Salome Kitomary, Mhariri wa Nipashe Digital, alishauri dira hiyo ianze kufundishwa mashuleni ili kuwajengea uelewa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa kuhusu nafasi yao katika kuitimiza.
Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema dira hiyo ina matumaini makubwa ya kutekelezeka kutokana na kasi ya maendeleo inayoonekana katika sekta muhimu kama barabara, reli, kilimo, maji na huduma nyingine za kijamii.
Mwisho
0 Comments