Na Moses Ng'wat, Ileje.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, leo Mei 20, 2025, amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya matengenezo ya sehemu korofi katika barabara ya Mapogolo–Mtima (km 2) na Mlale–Ikumbilo, zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Akiwa ameambatana na wataalamu kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Seneda amesisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara unapaswa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi, hususan kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani.
Kwa niaba ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Ileje, Mhandisi Emmanuel Mbulile alitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo na kubainisha kuwa thamani yake ni shilingi milioni 241.9, zikihusisha kazi katika barabara ya Mapogolo–Mtima na Ikumbilo–Mlale.
Mhandisi Mbulile alieleza kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya Ngongo & Sons kutoka Wilaya ya Mbozi, ambapo chanzo cha fedha ni kutoka Mfuko wa Barabara.
Alisema kazi zilizofanyika ni pamoja na kuinua tuta katika barabara ya Mapogolo–Mtima, kuumba tuta na kuweka kifusi katika maeneo korofi ya barabara ya Ikumbilo–Mlale na Mapogolo.
Aidha, alisema kazi ya ujenzi wa kalavati (box culvert) ipo katika hatua za mwisho, ikihusisha ujenzi wa maingilio na matoleo ya maji (wing walls), ili kuwezesha kupitika kwa barabara nyakati zote za mwaka.
Barabara ya Mapogolo–Mtima iliyopo Kata ya Mbebe Wilayani Ileje, ina umuhimu mkubwa kwani inaunganisha Tanzania na nchi jirani ya Malawi, hivyo kuboreshwa kwake kunatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri na biashara mpakani.
Mwisho.
0 Comments