WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa mwenendo wa biashara ya madini duniani umeendelea kubadilika kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na mahitaji ya soko.
Akiongea leo jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo Waziri kwakipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 amesema ,Katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025, bei ya madini ya dhahabu kwa wakia ilipanda hadi kufikia wastani wa dola za Marekani 2,655.80 ikilinganishwa na bei ya wastani wa dola za Marekani 2,078.09 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024.
Amesema Kuongezeka kwa bei ya dhahabu kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo mahitaji makubwa ya madini hayo duniani kama njia ya kuhifadhi thamani ya fedha.
"Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, mwenendo wa biashara ya madini ya almasi duniani umeendelea kukabiliwa na changamoto zinazosababishwa na mdororo wa uchumi wa dunia; uwepo wa almasi zinazotengenezwa kwenye maabara (Lab-Grown Diamonds) na kupungua kwa uhitaji katika masoko makubwa yakiwemo ya China na Marekani, " Amesema
Aidha, amesema bei ya madini hayo imeshuka kutoka wastani wa dola za Marekani 206.61 kwa karati mwaka 2023/2024 na kufikia dola za Marekani 168.95 kwa karati katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 sawa na upungufu wa asilimia 18.
"Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha wastani wa mauzo ulikuwa karati 281,021.99 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 47.48 ikilinganishwa na karati 164,837.94 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 34.06 katika kipindi kama hicho cha mwaka uliopita,"
Na kuongeza "Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, wazalishaji wakubwa wa almasi duniani wamepunguza uzalishaji ili kuimarisha bei," Amesema Waziri Mavunde
Aidha, kwa upande wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha biashara ya almasi kwa kuanzisha minada, maonesho, masoko na kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa madini ya almasi ndani ya nchi.
" Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na madini mkakati na madini muhimu (strategic and critical minerals) ambayo yanazidi kuhitajika duniani kwa ajili ya matumizi katika teknolojia za kisasa na nishati mbadala, " Amesema
Hata hivyo ameeleza kuw ,Mahitaji ya madini haya, yakiwemo lithium, cobalt, nickel, copper, aluminium, zinc, graphite, na rare earth elements (REE), yameendelea kuongezeka kutokana na jitihada za kimataifa za kupunguza hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050 (Net Zero Emission).
Amesema Kuongezeka kwa mahitaji haya kunatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa magari ya umeme, betri za kuhifadhi nishati, na vifaa vya teknolojia ya kisasa vikiwemo simu janja, darubini na kompyuta.
"Mheshimiwa Spika, hali hii inatoa fursa kubwa kwa Tanzania kuhakikisha madini haya yanaongezwa thamani ndani ya nchi ili kuongeza mapato, ajira, na mchango wake katika uchumi wa Taifa," Amesema .
Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje katika Sekta ya Madini, ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata madini haya ili kuyauza yakiwa yameongezwa thamani.
"Mheshimiwa Spika, ili kuongeza manufaa yatokanayo na madini muhimu na madini mkakati, Serikali imeendelea kuhimiza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kisasa cha usafishaji madini mbalimbali (Multi Metals Processing Facility) katika eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi la Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone) lililopo Wilaya ya Kahama," Amesema Waziri huyo.
0 Comments