Na Shomari Binda-Musoma
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma ( MUWASA) imewaita wananchi waliositishiwa huduma ya maji kuweza kurejeshewa.
MUWASA imefanya hivyo baada ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoa ofa ya wananchi waliokatiwa maji kurudishiwa pasipo kutoa faini na kuweka utaratibu wa kulipa deni.
Ofa hiyo ilitangazwa na Waziri wa maji Jumaa Aweso wakati akisoma bajeti ya Wizara hiyo kwenye Bunge la 12 kwenye Mkutano wa 19.
Akizungumza na Matukio Daima Mkurugenzi wa MUWASA mhandisi Nicas Mugisha amesema tayari wameanza kutekeleza ofa hiyo kwa wananchi.
Amesema wananchi waitumie fursa hiyo ambayo itamalizika mwishoni mwa mwezi huu kufika kwenye ofisi hizo ili kupata utaratibu mzuri wa kurejeshewa huduma kwa wale waliositishiwa.
Nicas amesema lengo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji karibu na makazi yao hivyo wapo tayari kutekeleza ofa hiyo.
Amesema kupitia mafundi wa mamlaka walionao watahakikisha wale wote watakaofika kwaajili ya huduma hiyo wanashughulikiwa.
" MUWASA tupo tayari kuwarejeshea huduma ya maji wale wote watakaofika kama ambavyo ofa imetolewa na mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na tunamshukuru sana.
" Wananchi wafike ofisini na tupo tayari kuwahudumia kuhakikisha wanapa maji kwenye makazi na siyo kuyafuata umbali mrefu",amesema.
Wakati huo huo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma ( MUWASA) juzi imepongezwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kwa kuwafikishia wananchi huduma bora ya maji.
Pongezi hizo zilitolewa na mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi wakati akisoma taarifa ya utekelezajj wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020/2025.
0 Comments