NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Wananchi wakazi wa Mji wa Mafinga wameitaka Serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kujenga Stendi mpya na kubwa ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba Mabasi yote ya abiria yanayopita mjini hapo.
Kauli hiyo imetokewa leo na wananchi, abiria na madereva wa mabadi yanayofanya safari kupitia barabara Kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Mbeya.
Wananchi hao walisema kuwa Mji wa Mafinga ni mmojawapo wa miji inayokua kwa kasi hapa nchini, na kuwa barabara Kuu inayokwenda mikoa ya Kusini imepita Mjini hapo.
"Kwa kweli ni aibu kubwa Mji kama huu wa Mafinga kuwa na Stendi kama hii, tufike mahali viongozi tuliowapa dhamana wajue kuwa stendi hii haifai kabisaa hata kuingiza mabasi", alisema Zakayo Kihongosi mkazi wa Mafinga.
Baadhi ya abiria walisema kuwa aina ya stendi ya Mafinga, haina hadhi inayoendana na umaarifi wa Mji wa Mafinga na kuongeza kuwa Serikali ijenge stendi yenye hadhi ili mabasi yote yaweze kuingia na kushusha abiria wake.
Wakizunguza na MATUKIO DAIMA MEDIA baadhi ya madereva wa mabasi yanayofanya Safari za mikoani na ndani ya wilaya ya Mufindi walisema kuwa stendi ya Mafinga ni uchochoro wa kihuni na haufai kuitwa stendi.
"Tunashangaa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Mafinga Mji wanashinda kuangalia tatizo la stendi hii, abiria wanashushiwa njiani suala ambalo ni hatari kupata ajali na kuibiwa na vibaka", alisema Makabe Mlape dereva wa Basi linalofanya safari za mikoani linalopita Mafinga.
Wananchi hao walisema Halmashauri ya wilaya ya Mufindi ni mojawapo ya wilaya ambazo zina mapato makubwa na vyanzo vingi vya rasilimali ambapo wanashindwa kuelewa wanakosea wapi hadi kushindwa kujenga stendi mpya yenye hadhi ya kuingiza mabasi yote.
MWISHO
0 Comments