Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Afisa Mtendaji wa Kata ya Rungwe Mpya halmashauri ya wilaya Kasulu Tausi Issa Manyanya amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma akikabiliwa na tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Manyanya alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo ya wilaya na kusomewa Shauri hilo la jinai namba CC 11711/2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo. Emaculate Shulli ambapo Mtuhumiwa anakabiliwa na makosa mawili chini ya kifungu cha 15(1)(a) na 15(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022.
Waendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) James Mosi Nyarobi na Bw. Davis Jason Junior Katika hati ya mashtaka walieleza kuwa Mtendaji huyo anadaiwa kuwa akiwa katika kijiji cha Rungwe Mpya wilaya ya Kasulu alidai na kupokea hongo ya shilingi 210,000 kutoka kwa mfugaji aliyetambulika kwa jina la Omari Haruna mkazi wa Kijiji cha Kigembe wilaya ya Kasulu.
Katika hati hiyo ya Mashitaka Mtenda huyo anadaiwa kupokea fedha hizo ili kuruhusu kurudishwa kwa ng’ombe mmoja wa mfugaji ambaye aliyepotea na kupatikana katika kijiji hicho Kigembe aliyekutwa amehifadhiwa kwa mfugaji, Longo Lugata Shija kwa maelekezo ya Afisa Mtendaji huyo wa kata.
Mtendaji huyo wa Kata ya Rungwe Mpya alikana mashtaka yote mawili yaliyosomwa mbele ya Mahakama hiyo ambapo Mahakama ilimpa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa, na shauri hilo limepangwa kusikilizwa tena tarehe 02, Juni mwaka huu.
Mwisho.
0 Comments