Ashrack Miraji Matukio Damia
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania. Mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi madhubuti wa Serikali, uwekezaji wa kimkakati, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa gesi.
Akizungumza katika kikao kazi kilichokutanisha Ofisi ya Msajili wa Hazina, Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kwenye hoteli ya Hyyat Regency jinini Dar es Salaam Mei 19, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Bw. Charles Sangweni, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutolewa kwa leseni ya uendelezaji katika eneo la ugunduzi la Ntorya—hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini. Pia alieleza kuhusu ukarabati wa visima vitano vya gesi, ambao umeongeza uimara na ufanisi wa uzalishaji.
Bw. Sangweni aliongeza kuwa PURA imeimarisha uhakiki na ukaguzi wa mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa Serikali inanufaika ipasavyo. Alisema pia kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa wazawa katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa vitalu vya utafutaji.
“Kampuni za kizawa zimeingia ubia na kampuni za kimataifa katika utoaji wa huduma za kitaalamu na kiteknolojia. Aidha, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika shughuli za mafuta na gesi yameongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisema Bw. Sangweni.
Alibainisha kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeimarika katika ukusanyaji wa data za mitetemo kwa ajili ya utafiti wa mafuta na gesi, na limewezesha pia tafiti za awali za kijiolojia, kijiofizikia na kijiokemia—hatua muhimu katika utafutaji wa rasilimali.
Bw. Sangweni alieleza kuwa PURA imeongeza ushirikiano wake na taasisi za udhibiti katika ukanda wa Afrika Mashariki. Vilevile, mfumo wa udhibiti wa sekta umeboreshwa kupitia uandaaji na usasishaji wa kanuni na miongozo ya kisheria.
“Majadiliano ya uwekezaji kwa mradi mkubwa wa kuchakata gesi kuwa kimiminika yanaendelea. Pia, idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 45 mwaka 2021 hadi kufikia 93 mwaka 2025, hali iliyosaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mkondo wa juu wa mafuta na gesi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa takwimu, katika kipindi cha Machi 2021 hadi Machi 2025, Tanzania imezalisha jumla ya futi za ujazo bilioni 301.33 za gesi asilia. Kati ya hizo, futi bilioni 142.35 zilitoka katika kitalu cha Mnazi Bay na bilioni 158.98 kutoka Songo Songo. Hii ni sawa na wastani wa futi bilioni 35.59 kwa mwaka kutoka Mnazi Bay na futi bilioni 39.74 kutoka Songo Songo.
Ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, uzalishaji wa gesi umeongezeka, ambapo awali Mnazi Bay ilikuwa ikizalisha wastani wa futi bilioni 32.03 kwa mwaka, huku Songo Songo ikizalisha futi bilioni 25.13 kwa mwaka.
Gesi hiyo imetumika katika matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, viwandani, majumbani, taasisi za umma na binafsi, pamoja na kwenye magari.
Kwa mujibu wa mikataba ya Ushirikiano wa Uzalishaji (PSA), mwekezaji huwekeza fedha zake mwenyewe katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi. Endapo atafanikiwa, hupata marejesho ya uwekezaji wake kupitia mgao wa mapato, kodi, tozo na hatimaye Serikali pamoja na TPDC hupokea mgao wao baada ya gharama hizo kutekelezwa.
PURA imeendelea kufanya uhakiki wa kina wa gharama na mapato ili kuhakikisha Serikali inapata mgao wake stahiki. Kupitia kaguzi hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 340 zimerejeshwa kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali na wawekezaji—fedha ambazo zingeweza kurejeshwa kwa wawekezaji kama sehemu ya mtaji wao.
Aidha, Serikali kupitia PURA imeanza maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vipya vya utafutaji wa mafuta na gesi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2013. Zoezi hili linatarajiwa kuvutia wawekezaji wapya na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
0 Comments