Na Mwandishi wetu .
NAINU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) uliofanyika leo, Mei 16, 2025, Jijini Kisumu, nchini Kenya.
Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, Mhandisi Kundo alisema mkutano huo umejikita katika kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya pamoja ndani ya Bonde la Ziwa Victoria, pamoja na kujadili mikakati ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi mipya ya maji.
“Mkutano huu umetupatia fursa ya kuangazia mafanikio ya miradi inayoendelea kutekelezwa, hususan ile inayohusisha nchi washirika, huku tukijipanga kutafuta rasilimali zaidi ili kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika ukanda huu,” alisema Mhandisi Kundo.
Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wa miradi ya LVBC, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya majitaka katika Jiji la Mwanza, pamoja na Mradi wa Kikanda wa Usalama na Uokoaji kwenye Ziwa Victoria.
Aidha, miradi mipya inayopendekezwa na kutafutiwa fedha inahusisha upanuzi wa huduma za majitaka katika Tanzania, Kenya na Uganda, miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Mkutano huo pia ulijadili kwa kina changamoto ya magugu maji katika Ziwa Victoria, ambapo mawaziri kutoka nchi wanachama walikubaliana kuchukua hatua za pamoja kupambana na tatizo hilo ambalo limekuwa likikwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayozunguka ziwa hilo. Sekretariati ya LVBC imeagizwa kuwasilisha mpango mkakati wa kutatua changamoto hiyo kwa haraka.
Mbali na Naibu Waziri wa Maji, ujumbe wa Tanzania pia uliwahusisha Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Khamis Hamza Khamis (Mb), na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb).
Baraza hilo la kisekta linajumuisha mawaziri kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na linawajibika kuratibu utekelezaji wa shughuli za Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria kwa manufaa ya wananchi wa ukanda huo.
Mwisho.
0 Comments