
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mkoani Simiyu Mhandisi Kundo Mathew ameanza kugawa pampu 100 za maji zenye thamani ya zaidi ya shilingi mil. 300 kwenye vijiji 84 vya Jimbo lake ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma ya Maji safi na salama.
Mhandisi Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, amesema anatambua changamoto za Wananchi kupata Maji, hivyo ametoa pampu hizo ili kuwarahishia wananchi kupata Maji kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na miradi ya serikali.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Mikutano Maalumu ya hadhara iliyofanyika katika kata za Mwaumatondo na Ihusi wilayani humo jana, Mhandisi Kundo amesema kwa kushirikiana na serikali wanaendelea kuwafikishia wananchi huduma ya Maji ambayo ni hitaji la msingi kwa binadamu.
Amesema licha ya kata ya Mwaumatondo kuwa Mradi wa Maji wenye thamani ya shilingi mil.300, ametoa pampu tatu katika vijiji vya Mwaumatondo, Mwabalizi na Mwasinasi ili wananchi wapate huduma ya Maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na Mradi huo.
"Katika kata ya Mwaumatondo, kuna wengine wana visima lakini hawana pampu, Diwani uliomba pampu tatu za Mwabalizi, Mwasinasi na Mwaumatondo...nimekuja nazo tatu, hizo hapo...hapa Ihusi nawapatia pampu nne ili zifungwe kwenye visima na Wananchi sasa wapate Maji safi na salama" amesema.
Ameeleza kuwa pampu hizo, zinatolewa na kukabidhiwa kwa kila tawi (Kijiji) ili kuwapunguzia wananchi michango, badala yake wajikite kwenye shughuli za kujiletea Maendeleo.
Ameongeza kuwa kupitia maombi Wananchi wa Kata hizo ambao waliona uhitaji wa kutumia pampu za Maji, hivyo akiwa Naibu Waziri wa Maji ilimwomba Rais Dk. Samia ili kupata pampu za Maji ambazo watazigawa pambu tatu Kwa kata ya Mwaumatondo na pampu nne kata ya Ihusi.
Mhandisi Kundo ameishukuru Rais Dk. Samia kwa kumpatia pampu 100 za Maji ambazo zitasambazwa Jimboni kwake ili kuwarahishia wananchi kupata huduma ya Maji safi na salama.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wilaya ya Bariadi, Moses Mwampunga amesema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Maji ambayo ni endelevu katika maeneo yao.
Amesema watahakikisha wanasimamia uendelevu wa huduma hiyo ya Maji ambapo pampu hizo ni chanzo kwa maeneo ambayo hayana Maji, huku aliongeza kuwa Pampu hizo 100 zitagawiwa kwenye viijij vyote 84 na zimegarimu zaidi mil 300, huku pampu moja ikigharimu shilingi mil 3.5.
Wananchi wa Kata hizo wamemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kununuliwa pampu hizo ambazo zitawarahisishia kupata Maji safi na salama.
Silya Kinya, mkazi wa Mwaumatondo ameishukuru serikali kupitia Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuwapatia huduma ya Maji ikiwemo pampu za mkono ambazo zitawawezesha kupata Maji safi na salama.
Mhandisi Kundo, leo ataendelea na ziara ya kufanya mikutano Maalumu ya kusoma Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025 katika kata za Gibishi na Nkindwabiye.
Mwisho.
0 Comments