NA Zuhura Zukheri Matukio daima, Iringa.
Mbunge wa Jimbo la Isimani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amekabidhi gari la wagonjwa (ambulance) katika Kituo cha Afya Isimani, kilichopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa tukio la kukabidhi gari hilo, Waziri Lukuvi alisema lengo la kukabidhi gari hilo ni kuharakisha usafiri wa wagonjwa wa dharura wanaohitaji kupelekwa Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Alibainisha kuwa kituo hicho kwa sasa kinatoa huduma za upasuaji, hivyo uwepo wa gari la dharura ni jambo la msingi katika kuokoa maisha ya wananchi.
“Kituo hiki kimepandishwa hadhi kutokana na kupokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali, hata kutoka nchi jirani, kwa kuwa kipo kando ya barabara kuu ya Iringa–Dodoma.
Serikali kupitia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeleta vifaa tiba vya kisasa ili huduma zinazotolewa ziwe bora na za kuaminika,” alisema waziri Lukuvi.
Aidha, waziri Lukuvi alieleza kuwa serikali imeridhia kuanzisha Kituo kingine cha Afya chenye hadhi katika eneo la Kisinga, Isimani, na tayari fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho zimepatikana. Alisema uamuzi huo umetokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za afya katika maeneo hayo na dhamira ya serikali ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Isimani Dkt Hussen Said alisema ujio wa gari hilo utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya usafirishaji wa wagonjwa, kwani awali walilazimika kuomba magari kutoka vituo vya jirani, ambayo mara nyingi yalikuwa tayari katika matumizi.
“Mara nyingine tulilazimika kutumia usafiri wa kawaida hata kwa wagonjwa waliokuwa katika hali mbaya, jambo ambalo lilihatarisha maisha yao. Kwa kweli tunaiona nuru mpya katika utoaji wa huduma baada ya kupokea gari hili,” alisema Dorice Kinyoa msimamizi wa kituo cha afya Isimani.
Wananchi wa Isimani walielezea shukrani zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mbunge wao Lukuvi na Diwani wa eneo hilo, kwa kuhakikisha gari hilo linapatikana. Waliwahimiza wananchi wenzao kulitumia kikamilifu Kituo cha Afya Isimani kwa kuwa sasa huduma zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Constantino Kihwele, alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge Lukuvi kwa namna anavyosimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka mitano mfululizo bila kuyumba.
Alisema waziri Lukuvi ni kiongozi mwenye busara, anayetoa ahadi na kuzitekeleza kwa wakati, jambo linaloendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa chama hicho.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jimbo la Isimani limenufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu, miundombinu, maji na afya yote yakiwa ni matokeo ya usimamizi thabiti wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mbunge wao mahiri.
0 Comments