Header Ads Widget

DKT BITEKO KUONGOZA HAFLA MIAKA 35 YA TAWLA

Na Irene Mark, Matukio Daima Blog 

NAIBU Waziri Mkuu Dotto Biteko, anatarajia kuongoza wanachama wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na wadau wa Sheria kwenye kilele cha miaka 35 ya mafanikio ya chama hicho.

Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, atashiriki ufunguzi wa hafla ya miaka 35 ya TAWLA leo Mei 22, 2025 huku akitarajia kusikia mafanikio na changamoto za wanasheria hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu miaka 35 ya chama hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile alisema maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

"TAWLA ilianzishwa mwaka 1989 na kusajiliwa rasmi mwaka 1990 sasa tangu wakati huo mpaka sasa tumetoa msaada wa kisheria kwa wananchi zaidi ya milioni saba.

”TAWLA imekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za wanawake na watoto wa kike hapa nchini, kupitia huduma za msaada wa kisheria, utetezi wa kisera na kisheria, elimu kwa umma na tafiti mbalimbali.

”Sherehe hizi ni fursa ya kutafakari safari iliyopita, mafanikio yaliyopatikana, na mikakati ya baadaye ya kuendelea kupigania usawa wa kijinsia na haki kwa wote,” amesema Mwambipile.

Pia chama hicho kimesema huduma wanazozitoa zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia wanawake na watoto kupata haki zao kwa njia ya kisheria, kuimarisha uelewa wa sheria katika jamii na kupunguza ukatili wa kijinsia.

Katika maadhimisho hayo, TAWLA imependekeza kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 na 17 ili kulinda haki ya mtoto wa kike chini ya miaka 18 na kumuepusha na ndoa za utotoni.

Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI