Na Matukio Daima App.
MBEYA.Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili wote wanawake ambao ni Seva Simwinga [29] na Sara Simwinga [35] wafanyabiasha na wakazi wa Mponja Uyole Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na shehena ya dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Kilogram 320.
Akizungumzia kukamatwa kwa watu hao, kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema watuhumiwa walikamatwa Mei 21, 2025 majira ya usiku katika operesheni maalum iliyofanywa na Jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya huko katika Mtaa wa Mponja uliopo Kata ya Uyole, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya.
Ameeleza kuwa watuhumiwa hao walikutwa na magunia 4 na masanduku 4 yenye dawa hizo za kulevya wakiwa wamehifadhi ndani ya nyumba wanamoishi.
Pamoja na hilo Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa pia Jeshi la polisi Mbeya linawashikilia Billy Mtafya [19] fundi magari, mkazi wa Uyole Jijini Mbeya na Joseph Nyalusi [25] kondakta wa Basi, mkazi wa Dodoma wakiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa Kilogram 30.
Amesema watuhumiwa walikamatwa kati ya Mei 19 – 20, 2025 saa 8 usiku katika kizuizi cha Polisi kilichopo katika eneo la Mpakani katika barabara kuu ya Mbeya Njombe Wilayani Mbarali wakiwa na mabegi manne na sanduku moja yakiwa yamefungwa na mifuko ya nylon ndani yake yakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi wakisafirisha kama mzigo katika Mabasi ya abiria yenye namba za usajili T.683 ELK aina Yutong mali ya kampuni ya ABC Upper Class na Basi namba T.385 EEU aina ya Yutong mali ya kampuni ya Shabiby Class yaliyokuwa yakitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kamanda Benjamin Kuzaga, linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani haina nafasi katika jamii na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo makini kuwabaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara hiyo. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa jamii kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
MWISHO.
0 Comments