Header Ads Widget

BODI YA ITHIBATI YAWAONYWA WANAOJIPENYEZA KWENYE TAALUMA YA HABARI

 


Na Fatma Ally Matukio DaimaApp 


Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya waandishi wa habari (JAB) Tido Mhando amewaonya wanaotaka kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa za usajili za kupatiwa kitambulisho cha uandishi wa habari (Press Cards).


Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kufunguliwa rasmi kwa mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa https://taihabari.go.tz


Amesema kuwa, bodi hiyo itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote wenye sifa kupitia mtandao na kutoa vitambulisho kidigital ambapo maombi yote yatafanyika kupitia mfumo unaoitwa TAI-Habari.


 "Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiitali (digital Press Card). Maombi ya ithibati Press Cards yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari" amesema.


Amesema kuwa, mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000).


Ameongeza kuwa, mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi.


Mhando amesema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.


Sambamba na hayo, amewaomba wahariri, waandishi na wadau wote wakiwemo waajiri kutambua umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na hivyo watoe ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo muhimu kwa taifa.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula amesema sheria ilitoa muda wa miaka mitano kwa waandishi ambao hawana vyeti kwenda kusoma ili waweze kukidhi vigezo vilivyowekwa kisheria.


Amesema baada ya muda huo kuisha Waziri aliongeza muda wa mwaka mmoja na kwamba tangu Waziri aongeze mwaka mmoja ni miaka miwili imeshapita na kufanya jumla ya miaka nane na hivyo hakutakuwa na muda wa nyongeza tena.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI