Na. Jacob Kasiri - Ruaha.
Wananchi walioingiza mifugo kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha Mei 07, 2025 wamekiri kuingiza mifugo hiyo na kuahidi kutorudia tena na kuwa walimu wa kuelimisha wenzao juu ya athari zinazosababishwa na ng’ombe ambazo zimeendelea kuleta madhara makubwa katika ikolojia na ustahimilivu wa Mto The Great Ruaha.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Kanali Maurid Surumbu alisema kuwa licha ya mzee Igembe Mahola aliyekuwa na Ng’ombe 527 hifadhini kukabidhiwa mifugo hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu, hivyo ni wajibu wa kila mfugaji kutii sheria zilizotungwa na Bunge zinazosimamia maeneo haya nyeti kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Kanali Surumbu alisisitiza, “Kwa wananchi wa vijiji 17 na Vitongoji 47 mnaoishi kando kando ya hifadhi hii na mnaomiliki mifugo, ikitokea kwa bahati mbaya au makusudi mmeingiza mifugo yenu hifadhi ni muhimu kujizuia kuanzisha mapambano na jeshi letu la uhifadhi kwa kuwa hatuna historia ya mifugo iliyokamatwa na TANAPA kufa au kupotea katika wilaya yetu ya Mbarali.”
Hifadhi ya Taifa Ruaha yumkini imeendelea kukumbwa na kadhia ya uingwizaji wa mifugo unaotishia mustakabali wa uhifadhi wa vyanzo vya maji na maisha ya bioanuwai licha ya maazimio kadhaa yaliyoafikiwa na vikao mbalimbali vilivyofanyika kati ya TANAPA, uongozi wa Wilaya ya Mbarali, Chama cha Wafugaji na wafugaji wenyewe juu ya kutoingiza mifugo ndani ya hifadhi hiyo.
Kwa taarifa iliyotolewa katika kikao kimojawapo cha Septemba 11, 2024 na uongozi wa wilaya hiyo, wilaya ya Mbarali ina jumla ya mifugo laki 388,109 huku ng’ombe pekee wakiwa ni 233,049 huku eneo la malisho likiwa ni hekari 154,000. Ili kukabiliana na upungufu wa malisho wananchi wanapaswa kubadilika na kufuga kisasa na si kupeleka mifugo hifadhini.
Utitiri huu wa mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha una madhara makubwa kwa wanyamapori, mbali ya magonjwa pia huongeza ushindani wa malisho kati yao na wanyamapori kunakopelekea wanyamapori kuathirika zaidi kwa kukosa malisho bora na kuanza kunyong’onyea na hatimaye kufa.
Mathalani, ng’ombe mmoja mkubwa huitaji takribani eneo lenye la zaidi ya mita za mraba 50 kwa siku, kwa hesabu za kawaida ng’ombe 527 huchunga eneo lenye ukubwa wa takribani hekari 2,635 ambazo ni sawa na zaidi ya kilomita 26, na ng’ombe mmoja mwenye kilo 400 ili ashibe anahitaji zaidi ya kg 12, tukizidisha mara mifugo inayoingia katika bonde la Usangu kwa siku au mwaka, ndani ya miaka mitano ijayo hatutakuwa na bonde tena bali jangwa. Hivyo ni wajibu wetu sote kuyalinda maeneo hayo ili yawe na faida kwa watazania wote.
Akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA katika kukabidhi ng’ombe hao 527 chini ya uongozi wa kijiji cha Iyala Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Catherine Mbena anayesimamia Kitengo cha Mawasiliano TANAPA alisema,
“Vitendo hivi vya kuingiza mifugo hifadhini au aina yoyote ile ya ujangili unaofanyika ndani ya maeneo haya hurudisha nyuma malengo ya uanzishwaji wa taasisi hizi za uhifadhi kwani faida inayotokana na utunzaji wake imeendelea kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Aidha, Kamishna huyo aliongeza kuwa askari wa uhifadhi wanafanya jitihada kubwa kulinda rasilimali hizi usiku na mchana kuhakikisha zinaendelea kuwepo, hivyo wananchi waone umuhimu huo wa kushirikiana na TANAPA kwa kutoa elimu kwa wanavijiji wenzao kutunza tunu hizi.
Naye, Mzee Igembe Mahola na mwenzake Omongo Shibola walikiri ng’ombe wao kukamatiwa hifadhini wakichungwa na vijana, hata hivyo baada ya kukamilisha taratibu za kisheria kwa kusaidiwa na uongozi wa wilaya na mkoa tunashukuru TANAPA wametukabidhi ng’ombe wetu wakiwa na afya nzuri.
Mifugo hiyo iliyokamatwa Mei 07, 2025 katika eneo la Mjenje zaidi ya kilometa 26 ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha alikabidhiwa jana Mei 16, 2025 kwa mmiliki wa mifugo hiyo ambaye ni Mzee Igembe Mahola chini ya uongozi wa kijiji cha Iyala akiwepo Mwenyekiti na Mtendaji mbele ya Waandishi wa Habari na baada ya hapo walifanya mahojiano na Mkuu wa Wilaya Mbarali Mhe. Kanali Maurid Surumbu kuhusiana na tukio hilo.
0 Comments