Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Zaidi ya shilingi Bilioni 50 za kitanzania zinatarajia kutumika kwa ajili ya kurudisha mazingira na uoto wa asili katika maeneo ya wilaya tatu za mkoa Kigoma ambayo yaliharibiwa na ujio wa wakimbizi mkoani humo.
Mkurugenzi wa mazingira ofisi ya Makamu wa Raisi,Kemilembe Salome Mutasa alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa miaka mitano wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi mradi unaotekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira (UNEP) kwa kushirkiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).
Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na uhifadhi na utunzaji mazingira kurudishwa kwenye asili yake kwa maeneo yaliyokumbwa na uharibifu wa mazingira alisema kuwa mradi huo pia unalenga kutoa elimu ya matumizi endelevu ya mazingira na upanda miti mpango unaolenga kutoa fursa ya kuvuna hewa ukaa kupitia kwenye mradi huo.
Akizindua mradi huo, Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa wimbi la wakimbizi kutoka nchi za maziwa makuu limekuwa na athari kubwa kwa utunzaji na uhifadhi wa mazingira kutokana na ukataji mkubwa wa miti kama nishati kuu ya kupikia sambamba na kuingia kwenye maeneo ya uhifadhi wa misitu na kuendesha shughuli za kilimo wakishirikiana na Watanzania wenyeji.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP),Paz Lopez - Ray alisema kuwa mradi huo unakuja kukiwa na changamoto kubwa ya uharibifu waa mazingira unaogusa pia changamoto za kiuchumi kwa wananchi na wakimbizi katika wilaya za Kasulu,Kibondo na Kakonko.
Lopez – Ray Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia masuala ya kilimo, uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji, kulinda mazingira, baianuai lakini kusaidia kusaidia masuala ya kiuchumi kwa wananchi 570,000 wanaozunguka maeneo yanayohifadhi wakimbizi na wakimbizi.
0 Comments