Na Moses Ng’wat, Tunduma.
Mvutano mkali kati ya madereva wa bajaji na Jeshi la Polisi umeibuka mjini Tunduma, mkoani Songwe, baada ya zaidi ya madereva wa bajaji 1,000 kufunga barabara kuu wakipinga kile walichokiita kunyanyaswa na kunyimwa haki ya kutumia barabara hiyo kwa shughuli zao za kila siku.
Tukio hilo ambalo lilizua taharuki kubwa baada ya polisi kulazimika mabomu, lilitokea leo Mei Mosi 2025, baada ya madereva hao kuziba barabara kwa kupanga bajaji zao.
Walijaribu kushunikiza serikali ipunguze msongamano wa malori kwani yamekuwa yakiziba barabara kwa muda mrefu yanaposubiri kuruhusiwa kuvuka kwenda Zambia hali ambayo huwaletea usumbufu, ikiwemo kutaka jeshi la polisi ifute baadhi ya vituo vya ukaguzi wa usalama barabarani.
“Tumechoka. Polisi wanatulazimisha kutumia barabara ya zamani isiyo na hadhi wala abiria wa kutosha, tunahitaji kupewa nafasi sawa kama watoa huduma wengine,” alisema Yona Mwakajinga, mmoja wa madereva waliokuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo.
Amani Mwaipaja, dereva mwingine, alieleza kuwa foleni ya malori iliyopangwa kwa njia tatu kwenye barabara kuu imekuwa kikwazo kikubwa kwao, na kwamba wanataka serikali iagize foleni hizo zielekezwe njia mbadala ili kupunguza msongamano.
Mwenyekiti wa madereva bajaji Tunduma, Mwinyihaji Kumbao, alisema kuwa hatua ya kuwazuia kutumia barabara kuu siyo tu inazorotesha uchumi wao bali pia ni kunyimwa haki ya kufanya kazi kwa uhuru katika mji wao.
Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, Charles Bukombe, alijitokeza eneo la tukio kuwasihi madereva hao kufungua barabara na kutoa nafasi kwa mazungumzo, lakini waligoma, hali iliyolazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na kurejesha utulivu.
0 Comments