Na,Jusline Marco;Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka waandishi wa habari nchini kuitumia Akili Mnemba (A I) kama chombo cha kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi, na siyo kama kikwazo cha uhuru wao wa kufanya kazi.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2025 yaliyofanyika jijini Arusha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa teknolojia mpya kama AI inapaswa kupewa nafasi katika tasnia ya habari ili kuongeza ubunifu, ufanisi na kufikia jamii kwa haraka zaidi.
Aidha metoa wito kwa wanahabari kuendelea Kudumisha maadili ya utangazaji na uandishi wa habari , Kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi, Kutoa taarifa zinazojenga jamii na kuleta matokeo chanya Pamoja na Kutangaza mafanikio ya serikali kwa uwazi na uadilifu
Ameongeza kuwa uhuru wa vyombo vya habari lazima ulindwe, huku akisisitiza kuwa hakuna uhuru usio na mipaka, ukizingatia maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, ametoa wito kwa waandishi wa habari kubadilika na kuandika habari zenye kujenga jamii badala ya zile zenye kuchochea migogoro au kueneza hofu huku akisema kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuunda taswira na mwenendo wa jamii kupitia kazi zao.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari, chini ya kaulimbiu isemayo Uhabarishaji kwenye dunia mpya: Mchango wa Akili Unde kwenye uhuru wa vyombo vya Habari"na ujumbe mkuu ukiwa ni kulinda na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya taifa.
0 Comments