Header Ads Widget

WATUNISIA WAANDAMANA KUPINGA UKANDAMIZAJI WA RAIS SAIED DHIDI YA UPINZANI

Maelfu ya raia wa Tunisia wanaandamana jijini Tunis wakipinga ukamataji wa wapinzani na wanaharakati, huku wakimtuhumu Rais Kais Saied kwa kuendeleza utawala wa kidikteta na kukandamiza uhuru wa kisiasa.

Waandamanaji walijitokeza kwa wingi kuanzia Ijumaa wakibeba mabango yenye picha za waandishi wa habari, wanasiasa na mawakili walioko jela, wakiimba: "Ni zamu yako Saied, dikteta" na "Wananchi wanataka kuuangusha utawala."

Maandamano hayo yamechochewa na kukamatwa kwa wakili maarufu Ahmed Souab, mkosoaji mkubwa wa serikali, pamoja na hukumu kali zilizotolewa kwa viongozi wa upinzani wiki iliyopita, baadhi yao wakipewa vifungo vya hadi miaka 66 jela kwa madai ya kula njama dhidi ya taifa.

Waandamanaji walitembea kutoka makao makuu ya Chama cha Waandishi wa habari hadi barabara ya Habib Bourguiba, wakiungwa mkono na vyama vya siasa, wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika ya kiraia.

Serikali ya Rais Saied inatuhumiwa kutumia mahakama kama chombo cha kisiasa, hasa baada ya kuvunja Bunge mwaka 2021 na kuanza kutawala kwa amri.

Mnamo 2022, alivunja pia Baraza Kuu la Mahakama huru na kufukuza majaji kadhaa hatua iliyotajwa kama mapinduzi ya kimyakimya na wapinzani.

Wakati huo huo, mataifa ya Ufaransa, Ujerumani na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wameikosoa vikali Tunisia kwa ukiukaji wa haki za washitakiwa na kutozingatia misingi ya haki wakati wa hukumu hizo.

Rais Saied aliwahi kuwaita wapinzani wake "wasaliti na magaidi", akionya kuwa majaji wanaowaachia huru ni "washirika wao".

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI