Header Ads Widget

"HAKUNA ALIYE JUU YA SHERIA"- RAIS SAMIA AWAONYA WANASIASA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria, akisisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kuhakikisha kuwa amani ya taifa inalindwa wakati wote.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya kutokea mvutano mkali kati ya Jeshi la Polisi na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, waliokusanyika katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Aprili 24, 2025, kwa lengo la kuhudhuria kesi ya mwenyekiti wao, Tundu Lissu.

Kwa mujibu wa CHADEMA, vurugu hizo zilisababisha kukamatwa kwa viongozi waandamizi wa chama hicho akiwemo Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu John Mrema, huku wakidai kuwa mtu mmoja alipoteza maisha na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Chama hicho kilionyesha baadhi ya majeruhi mbele ya wanahabari pamoja na wawakilishi wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, na Chama cha Mawakili kutoka Kenya.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi halijathibitisha moja kwa moja madai ya kifo hicho wala majeruhi waliotajwa. Polisi ilieleza kuwa mwanaume mmoja ambaye hakufahamika jina wala makazi alikutwa katika eneo la Coco Beach akiwa hajitambui, na baadaye alibainika kuwa amefariki dunia. Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, uchunguzi wa chanzo cha kifo unaendelea.

Kwa muda sasa tangu uongozi wa Lissu uinge madarakani mwezi Januari, 2025, CHADEMA kimeendelea kushikilia msimamo wake wa "No Reform, No Election", kikisisitiza kuwa hakutakuwa na uchaguzi hadi pale kutakapofanyika marekebisho makubwa ya sheria na mifumo ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.

Msimamo huo umepelekea kukamatwa kwa Lissu ambaye sasa anakabiliwa na kesi mbili tofauti za uchochezi na uhaini. Kwa sasa, anashikiliwa rumande kwa kuwa shtaka la uhaini halina dhamana kisheria.

Picha zilizosambazwa na chadema, kuonyesha majeruhi waliyopata wafuasi wao baada ya kukinzana na Polisi

Akilihutubia taifa kupitia televisheni, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza siasa kwa njia ya amani na kwa kuzingatia sheria.

"Wote tunapaswa kuendesha shughuli zetu za kisiasa tukizingatia kuwa amani na usalama wa nchi ndiyo kipaumbele chetu cha kwanza," alisema.

Aidha, aliwaonya wanasiasa na wafuasi wao dhidi ya kuchochea migogoro ndani au nje ya vyama vyao, akisema:

"Kamwe tusiruhusu uchaguzi huu kuwa chanzo cha migogoro, chuki, mivutano na uvunjifu wa amani ndani ya vyama, baina ya vyama au nchini kwa ujumla."

Katika hotuba hiyo hiyo, Rais Samia alisisitiza kuwa demokrasia ya Tanzania imeendelea kukua na kuimarika, hasa kupitia falsafa ya R4 inayosisitiza kujenga maridhiano ya kisiasa na kijamii miongoni mwa Watanzania, kuimarisha ustahimilivu wa kitaifa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, kufanya maboresho ya kisera, kisheria na kiutendaji, pamoja na kujenga upya taasisi na mifumo ya utawala kwa misingi imara na ya haki.

Rais Samia alisisitiza kuwa utekelezaji wa falsafa hiyo lazima uende sambamba na kuheshimu Katiba na sheria za nchi, kwani ndizo msingi wa amani na utawala wa sheria.

Hotuba hiyo ya Rais Samia ilitolewa katika muktadha wa kuelekea Maadhimisho ya Miaka ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo kila Aprili 26, Tanzania huadhimisha siku hiyo muhimu.

Mwaka huu, taifa linaadhimisha miaka 61 ya Muungano tangu nchi hizo mbili ziungane rasmi mwaka 1964.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI