Header Ads Widget

TANZANIA YAONDOA ZUIO LA BIASHARA YA MAZAO KATI YAKE NA MALAWI NA AFRIKA KUSINI



 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo imetangaza rasmi kuondoa zuio lililowekwa hivi karibuni kuhusu biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo kati ya Tanzania na nchi za Malawi na Afrika Kusini.

Zuio hilo lilitangazwa tarehe 23 Aprili 2025 kwa lengo la kudhibiti uingizwaji wa mazao katika mipaka ya Tanzania baada ya Malawi kutangaza hatta kama hiyo.

Hata hivyo, kutokana na mawasiliano na majadiliano ya haraka kati ya serikali ya Tanzania na serikali za Malawi na Afrika Kusini, pamoja na ushirikiano wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mambo ya Nje, imeamuliwa kuondoa zuio hilo kuanzia Leo tarehe 26 Aprili 2025.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein M. Bashe, serikali ya Malawi imeahidi kuleta ujumbe maalum jijini Dodoma tarehe 2 Mei 2025 kwa ajili ya majadiliano zaidi kuhusu afya ya mimea na masuala ya masoko.

Aidha, majadiliano na wataalam wa Tanzania na Afrika Kusini yanaendelea ili kuhakikisha maslahi ya afya ya mimea na usalama wa mazao yanalindwa.

Serikali ya Tanzania imewahakikishia wakulima na wafanyabiashara nchini humo kuwa uhuru wa biashara ya mazao utaendelea kulindwa kwa kuzingatia viwango vya afya na usalama wa mimea, huku ikizingatia manufaa ya kiuchumi na kidiplomasia kwa pande zote.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI