Header Ads Widget

VIPAUMBELE VYA TANAPA 2025/2026 NI ULINZI, MIUNDOMBINU, MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA MAZAO MPYA YA UTALII


Na. Andrew Mbai - Mto wa Mbu.

Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) inayoongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Juma Nassoro Kuji, imeweka vipaumbele muhimu katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2025/2026 ili kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii. 

Vipaumbele hivyo vimewekwa katika kikao kazi cha Menejimenti ya Shirika  kilicholenga kujadili maandalizi ya mwisho ya bajeti ya Shirika kwa mwaka mpya wa fedha wa 2025/2026. Kikao hicho kimefanyika jana Aprili 04, 2025 katika ukumbi wa mikutano uliopo Hifadhi ya Taifa Manyara.

Akizungumza na washiriki wa kikao, Kamishna Kuji alieleza dhima ya Shirika katika kutengeneza bajeti inayoangazia vipaumbele vinavyotatua changamoto na kuboresha utendaji na utekelezaji wa majukumu ili kufikia malengo ya Shirika na Taifa kwa ujumla.



“Mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 tunaweka mkazo katika kuongeza nguvu kwenye shughuli za ulinzi na usalama wa hifadhi, kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii, kuboresha upatikanaji na uboreshaji wa vitendea kazi kama vile kupata magari kwa ajili ya doria na kukarabati magari yenye uhitaji huo.” alisema Kamishna Kuji

Pia, Kamishna Kuji alisisitiza kutengeneza bajeti itakayolenga kutoa msukumo katika uanzishaji wa mazao mapya ya utalii ili kuongeza mapato ya Shirika na Taifa, ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za uhifadhi, matumizi ya teknolojia, utatuzi wa migogoro kati ya wanyamapori wakali na waharibifu na binadamu sanjali na kuboresha  maslahi kwa watumishi.

Wajumbe wa kamati ya bajeti ya Shirika wilipata fursa ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Shirika inayoendelea ya mwaka  2024/2025 ambapo walibainisha maeneo ya msingi ambayo yametekelezwa kwa ufanisi ikiwemo kuhamasisha watanzania kuchangamkia fursa ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea Hifadhi za Taifa na Vituo vya Malikale vilivyokasimishwa kwa TANAPA.



Sambamba na hilo pia, Kamati ilieleza  maeneo mengine ya kuweka kipaumbele ni pamoja na kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu ya utalii na utawala ikiwemo matengenezo ya barabara zilizopo hifadhini, ujenzi wa malango ya utalii na ujenzi wa hosteli zinazotumiwa na wanafunzi wanapotembelea Hifadhi za Taifa, udhibiti wa mimea vamizi, udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu, utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo.

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Sekela Mwangota, ambaye ndie Katibu wa Kamati ya Bajeti ya Shirika alielezea namna bajeti mpya ilivyoandaliwa.

“Uandaaji wa mapendekezo ya bajeti ya Shirika kwa mwaka wa fedha 2025/2026 umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali wa Mwaka 2025/2026, Mpango Mkakati wa Shirika, Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali za nchi, vipaumbele vya Shirika na Nchi pamoja na maelekezo mahsusi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayolenga kuboresha ustawi wa jamii ya watanzania” alieleza Kamishna Sekela.

Mapendekezo ya Bajeti ya Shirika kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yatawasilishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi kwa ajili ya uchambuzi na idhini kabla ya kuanza kutumika rasmi mnamo tarehe 01.07.2025.

Shirika linaendelea kutekeleza majukumu yake ili  kuhakikisha kuwa uhifadhi endelevu wa maeneo yote yaliyotengwa kuwa hifadhi za Taifa nchini unaimarika kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI