Na Matukio Daima Media
Diwani wa Kata ya Mtwango, Monte Edson Kilamlya, ameiomba Serikali kuongeza nguvu katika ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nyololo hadi Ziro Ziro, pamoja na kutoka Mgololo kwenda Mafinga, akieleza kuwa barabara hizo zimekuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu.
Ombi hilo amelitoa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa miche bora ya parachichi 139 kwa mabalozi na wenyeviti wa vitongoji katika Kijiji cha Sawala. Zoezi hilo linahusisha pia vijiji vya Kibao, Lufuna, Mtwango, Lufuna na Kitiru, likiwa ni ishara ya kutambua mchango wa viongozi hao wa mitaa.
Monte alisema kuwa ameamua kugawa miche hiyo kama ishara ya shukrani kwa mabalozi na wenyeviti wa vitongoji ambao wanafanya kazi kwa kujitolea licha ya kutolipwa mishahara. Alieleza kuwa katika kata ya Mtwango kuna mabalozi 21 na vitongoji 6, na kwamba ameamua kuwaenzi kwa kuwapatia miti hiyo yenye manufaa ya kiuchumi.
"Miche hii ikitunzwa vizuri na kuanza kuzaa, itakuwa msaada kwa viongozi wetu. Watapata matunda kwa matumizi ya nyumbani na pia kuuza ili kujiongezea kipato. Nimeona ni vyema kutoa zawadi hii yenye manufaa ya muda mrefu badala ya vitu kama sukari ambavyo huisha haraka," alisema Monte.
Akizungumzia maendeleo ya kijiji cha Sawala, Monte alieleza kuwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, wamepokea fedha mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ikiwemo madawati 110 na mifuko ya saruji kupitia nguvu ya Mbunge wao.
"Serikali pia imelenga kuboresha miundombinu ya vyoo katika shule ya msingi ya Sawala, ambavyo tayari vimekamilika na vimeanza kutumika. Naendelea kusisitiza ombi letu la barabara ya Nyololo hadi Ziro Ziro na Mgololo hadi Mafinga; barabara hizi ni muhimu sana kwa wananchi wa Mtwango," alisisitiza.
Monte aliongeza kuwa Halmashauri imetenga Shilingi milioni 54 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo, ambapo tayari ujenzi wa wodi ya akinamama na watoto umeanza.TAZAMA VIDEO BOFYA LINK HII
.
0 Comments