NA MATUKIO DAIMA MEDIA, Mufindi
MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mufindi, Jasmine Ng’umbi, amewahimiza vijana kote nchini kutumia nguvu ya mitandao ya kijamii kupambana na wapotoshaji wanaobeza juhudi na mafanikio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na Matukio Daima Tv kipindi Cha Tanzania ya Leo ,Jasmin alisema kuwa wakati huu taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, kumekuwa na ongezeko la taarifa za upotoshaji zinazoenezwa na baadhi ya watu, hususan wapinzani, kwa lengo la kufifisha mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita.
“Ni wakati wetu sasa kuutumia kwa manufaa ya taifa tusiwape nafasi wapotoshaji Wako wanaoeneza uongo kuhusu Serikali na juhudi za Rais wetu Ni jukumu letu kusahihisha upotoshaji huo kwa kutumia ushahidi wa picha na video kutoka kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Jasmin.
Alisema kuwa si sahihi kwa vijana kutumia muda mwingi kwenye mitandao kwa kusambaza habari zisizo sahihi au kujihusisha na mabishano yasiyo na tija, badala yake waitumie mitandao hiyo kama chombo cha kuelimisha na kuhamasisha maendeleo.
“Kama kuna shule imejengwa, hospitali imekarabatiwa, au huduma zimeboreshwa, twendeni tukapige picha, tupange ujumbe mzuri na tusambaze kwenye makundi ya WhatsApp, Instagram, Facebook na Twitter. Tuonyeshe kazi inayofanyika badala ya kupiga kelele zisizo na msingi,” alieleza.
Aidha, Jasmine aliwataka vijana wa UVCCM kuwa mfano wa kuigwa kwa nidhamu na uzalendo, si tu kwenye mitandao bali hata katika jamii.
Alisema mijadala mingi ya mitandaoni haipaswi kujibiwa kwa jazba, bali kwa ushahidi wa maendeleo unaoonekana.
Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita, Jasmine alisema kuwa Rais Samia ameweka msisitizo mkubwa katika kuboresha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya, miundombinu na uwezeshaji wa vijana.
Alitaja ongezeko la bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, barabara mpya, na upanuzi wa huduma za umeme vijijini kama baadhi ya mafanikio yanayopaswa kuenezwa kwa njia chanya.
“Serikali hii inafanya kazi kubwa sana, na kwa kweli Rais wetu ni kielelezo cha uongozi thabiti na wa kizalendo Vijana tusikae kimya, tusimame na kuonyesha kazi hizi. Kila mmoja wetu awe balozi wa maendeleo mahali alipo,” alihitimisha.
Kauli hiyo imeibua hamasa kubwa kwa vijana waliohudhuria kikao hicho, ambao walikubaliana kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kuanza mara moja kuibua na kuonyesha kazi za maendeleo zinazotekelezwa kwenye maeneo yao kupitia mitandao ya kijamii.
0 Comments