Tanzania inatishia kuzuia uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini ikionya pia kuzuia usafirishaji wa bidhaa za nchi hizo mbili kupitia Tanzania ikiwa masharti ya kibiashara dhidi ya mazao ya Tanzania hayataondolewa kufikia Jumatano ijayo.
Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe, kufuatia uamuzi wa Malawi wa kuzuia uingizaji wa bidhaa kutoka Tanzania kama vile unga, mchele, tangawizi, ndizi, na mahindi.
Wakati huo huo, Afrika Kusini imeendelea kuzuia uagizaji wa ndizi kutoka Tanzania, licha ya mazungumzo ya muda mrefu.
"Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupitia ndani ya mipaka ya Tanzania kuelekea Dar es Salaam au nchi nyingine yeyote, hadi kizuizi hicho kitakapoondolewa," alisema Bwana Bashe.
"Usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania," Taarifa ya Waziri imesema.
Nchi zote tatu - Tanzania, Malawi, na Afrika Kusini - ni washiriki wa Jumuiya ya Muungano wa Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC), ambazo zinaibua wasiwasi juu ya kuongezeka kwa mvutano ndani ya muungano huo.
0 Comments