Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akiwa amebeba tenga lenye magugumaji
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA
Serikali kupitia Wizara ya fedha inatarajia kutoa fedha ya dharura kiasi cha shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha huduma katika Ziwa Viktoria ikiwemo ununuzi wa mtambo wa uvunaji wa magugumaji utakaosadia kutatua na kumaliza changamoto hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda Aprili 28, 2025 alipotembelea eneo la Kigongo Ferry, Wilaya Misungwi lililoathirika na Gugumaji Jipya (Salvina Species) na kusababisha usafiri kuwa na changamoto.
Mtanda ameeleza kuwa swala la mashine ya kisasa ya kufyeka magugumaji halikwepeki kwa Taifa linalohitaji Maendeleo na kutatua changamoto zinazojitokeza sehemu mbalimbali na kusababisha kukaa Kwa muda mrefu.
Kwa upande mwingine Mtanda amezitaka Taasisi za kisekta kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kuhakikisha wanamaliza changamoto ya magugu maji katika ziwa victoria.
Mtanda amesema kuwa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu si la watu wa Bodi ya maji Bonde la Ziwa Viktoria bali hata Taasisi zingine kama vile Uvuvi kwa kuwa shughuli za uvuvi na ufugaji wa samaki zinafanyika katika ziwa hilo na Ujenzi kwa kuwa kuna shughuli za usafirishaji wa abiria kwa vivuko lakini pia Taasisi za Mazingira pia.
“Hapa kuna athari mbalimbali na sote tunahitajika katika kufanya usafi ziwani, hii shughuli sio ya Bonde tu bali Taasisi na Wizara zingine zinaweza kuathirika lazima muwekeze fedha ili shughuli hii iende vizuri”
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la ziwa Viktoria Dkt. Renatus Shinhu amesema kuwa mpaka sasa tayari tani 441 za magugu maji yameopolewa na shughuli hiyo inaendelea ikiwa ni mpango wa muda mfupi mpaka pale mtambo wa kuvuna magugu maji utakapofika kwa kuwa tayari andiko la kupata fedha limeshawasilishwa Wizara ya Fedha kwa utekelezaji.
Katika kipindi cha mwezi January 2025 ilishuhudiwa ongezeko kubwa la gugumaji jipya na kuanza kuleta athari mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi, ufugaji samaki (Vizimba-Luchelele na Bukumbi) na vyombo vya usafiri hususani vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi na kuzorotesha huduma ya usafiri kati mkoa wa Mwanza kwenda kwenye maeneo mengine yanayozunguka Ziwa ambayo yanategemea vivuko hivyo.
0 Comments