Na Matukio Daima Media
Naibu Meya wa Manispaaa ya Iringa Juli Sawani , ameelezea kwa kina sababu zilizochangia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya kitaifa ya afya na usafi wa mazingira, huku akifichua pia changamoto zilizowazuia kufika kileleni licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na viongozi wa mitaa, wananchi na taasisi mbalimbali ndani ya Mkoa huo.
Akizungumza na Matukio Daima TV, Sawani amesema kuwa kwa miaka mingi Manispaa ya Iringa imekuwa ikifanya vizuri kwenye suala la usafi na mazingira, lakini mwaka huu wamekosa baadhi ya vigezo muhimu ambavyo vingewapa nafasi ya kuibuka kinara.
"Vipo vigezo vingi vinavyozingatiwa ili Halmashauri husika iweze kushika nafasi nzuri ya usafi katika mkoa husika, Moja ya vigezo hivyo ni usalama wa vyoo bora katika maeneo yenu, usafi wa mazingira kwa ujumla, pamoja na namna madampo yenu yanavyotunzwa na taka zinavyokusanywa.
Haya ni mambo muhimu sana yanayoangaliwa Sisi kama mkoa tunajitahidi, japokuwa kwenye kigezo cha mabadiliko ya ukusanyaji taka kutoka madampo hadi kwenye magari, bado hatujafikia kiwango kizuri hasa kwa upande wa wananchi na hilo limekuwa changamoto kwa mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka jana."
Mbali na kuelezea changamoto zilizowakwamisha mwaka huu, Sawani pia amefunguka kuhusu mbinu walizopanga kuziimarisha ili kuhakikisha Mkoa wa Iringa unashika nafasi ya kwanza kitaifa katika usafi wa mazingira.
“Ili mji wa Iringa uweze kuwa safi, ni lazima kila kaya iwe na kontena la kuhifadhia taka, Kisha gari linapita na kupeleka moja kwa moja dampo. Hii ni muhimu kwa sababu watu wameongezeka sana, hivyo kama jamii tunatakiwa kulinda makontena yetu hadi gari la usafi litakapopita.”
Alisisitiza kuwa usafi wa kudumu hautafikiwa bila ushirikiano wa wananchi na uelewa juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kuanzia ngazi ya familia.
Aidha, Sawani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kihesa amezungumzia mchakato wa ujenzi wa soko jipya katika eneo hilo, akitoa ufafanuzi juu ya hofu iliyojitokeza miongoni mwa baadhi ya wananchi kuhusu kuondolewa kwa soko la sasa.
Ametoa hakikisho kuwa hakuna mwananchi atakayeachwa nyuma, na kwamba kila hatua ya ujenzi huo imezingatia ushirikishwaji wa jamii.
“Ujenzi wa soko hilo upo katika mchakato mzuri, Na uzuri ni kwamba wananchi wameshirikishwa ipasavyo, hasa kwenye uchaguzi wa ramani ya ujenzi. Ramani iliyotumika ni ile waliyopendekeza wenyewe, kwa hiyo ni soko lao, lililotokana na maoni yao pia ujenzi huo unalenga kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza usalama wa wafanyabiashara na kuhakikisha soko hilo linakuwa la kisasa, lenye huduma zote muhimu.
0 Comments