Header Ads Widget

MIRADI SITA YA MAJI YAUNGANISHIWA UMEME MEATU.

Tanki la Maji.



 Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.


MIRADI sita ya Maji iliyotekelezwa mwaka 2012/13, ambayo ilikuwa inatumia Nishati ya dizeli katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, imeunganishiwa Umeme kutoka gridi ya Taifa ili kurahisisha utoaji wa huduma na kupunguza gharama za uendeshaji.


Miradi hiyo ambayo ilitekellezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), ilikuwa inatumia Nishati hiyo kutokana na Umeme kutofika maeneo hayo.


Akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoani humo iliyofanyika juzi wilayani Meatu, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Emmanuel Luswetula amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 wameiboresha miradi hiyo kwa kuweka Nishati ya Umeme ili kuwa na uhakika wa huduma ya Maji.


Amesema wamekamilisha kuweka Nishati ya Umeme katika miradi ya Maji Itinje, Sakasaka na Nkoma lakini pia wanaendelea kuunganisha Umeme katika miradi ya Ng'hboko, Mwamalole na Mwangudo na utekelezaji wake utakamilika Mei 30, mwaka huu.


"Matumizi ya dizeli ni gharama kubwa katika uendeshaji wa miradi ya Umeme, tumeunganisha miradi hii kwenye Umeme wa gridi ya Taifa ili kurahisisha utoaji wa huduma pia kupunguza gharama za uendeshaji" amesema Mhandisi Luswetula.


Katika hatua nyingine, Meneja huyo amesema watahakikisha wanaendelea kusimamia Ubora wa miradi ya maji ili kuzingatia thamani ya fedha na Wananchi ili wapate huduma kwa wakati.


Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa (MNEC), Gungu Silanga ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kutekeleza miradi ya Maji katika Mkoa wa Simiyu ili kuwatua ndoo akina mama.


Aidha, Gungu ameitaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini, kuhakikisha wanasimamia Ubora wa miradi ya Maji kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.


Mwisho.


Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Emmanuel Luswetula, akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani).


Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa (MNEC), Gungu Silanga (katikati) akiongea kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Simiyu kilichofanyika wilayani Meatu, kulia ni Katibu wa CCM Mkoa huo, Eva na Ndegeleki na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Meatu Faudhia Ngatumbura aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI