Header Ads Widget

MAKUMI YA WATU WAFARIKI BAADA YA MVUA KUBWA KUNYESHA KATIKA MJI MKUU WA CONGO

 


Mvua kubwa na mafuriko imesababisha vifo vya takriban watu 33 huko Kinshasa - mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - kulingana na maafisa.

Wakazi waliokata tamaa wanajaribu kukimbia maji ya mafuriko kwa kuogelea, au kupiga kasia hadi mahali salama kwa mitumbwi iliyotengenezwa kienyeji.

Mji huo una wakazi milioni 17, na upo kwenye mto Congo, ambao ni mojawapo ya mito mikubwa zaidi duniani na umeenea kote nchini.

Mafuriko ni ya kawaida - hivi karibuni mto ulifikia kiwango chake cha juu zaidi katika miongo sita.

Sehemu za mji mkuu zinakabiliwa na mmomonyoko wa udongo na katika miaka ya hivi karibuni rais wa Congo ameonya kuwa mzozo wa mabadiliko ya tabianchi unafanya mafuriko kuwa mabaya zaidi.

Nyumba nyingi magharibi mwa Kinshasa zilisombwa na maji kufuatia mafuriko usiku kucha kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi.

Takriban nusu ya wilaya 26 za jiji zimeathirika kwa jumla, kulingana na meya wa mji mkuu, ambaye anasema timu za utafutaji na uokoaji zimetumwa.

Walioathirika zaidi ni maeneo yaliopo viungani mwa jiji hilo pamoja na baadhi ya vitongoji maskini zaidi.

"Maji yamefikia urefu wa mita 1.5. Tumefanikiwa kujiokoa, wengine wamenasa majumbani mwetu," Christophe Bola anayeishi eneo la Ndanu aliambia shirika la habari la AFP.

Wakaazi wengine wa eneo hilo wamewaambia waandishi wa habari kuwa wamekasirishwa na mamlaka, wakiishutumu kwa kutokuwa wepesi wa kujibu na kutotuma msaada wa kutosha.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI