Header Ads Widget

DAKTARI WA GAZA ALIYETOWEKA ANAZUILIWA NA ISRAEL- MSALABA MWEKUNDU

 

Shirika la Red Crescent la Palestina lilisema Assad al-Nassasra "alitekwa nyara kwa nguvu" na wanajeshi wa Israel mwezi uliopita na kutaka aachiliwe huru.

Daktari wa dharura wa Kipalestina, Assad al-Nassasra, ambaye alikuwa hajulikani alipo tangu shambulio la anga la Israel lilillouwa wahudumu wengine 15 wa huduma za dharura kusini mwa Ukanda wa Gaza takriban wiki tatu zilizopita, sasa anazuiliwa na mamlaka za Israel.

Taarifa hii imethibitishwa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC).

Kupitia taarifa rasmi, ICRC imesema imepokea taarifa kuwa Bw. al-Nassasra, ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Red Crescent la Palestina (PRCS), anashikiliwa katika kituo cha kizuizi cha Israeli.

PRCS kwa upande wake imesema daktari huyo “alitekwa kwa nguvu” na wanajeshi wa Israel baada ya shambulio hilo na imetoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja.

Hadi sasa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) halijatoa uthibitisho rasmi kuhusu kuzuiliwa kwa daktari huyo. Msemaji wa jeshi hilo amesema wanatambua taarifa zinazodai mahali alipo, lakini hawajathibitisha chochote hadharani.

Maiti za wahudumu wanane wa PRCS, wapokeaji huduma sita wa Ulinzi wa Raia, na mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa zilipatikana katika makaburi ya juujuu kandokando ya mji wa Rafah, wiki moja baada ya msafara wao kushambuliwa na vikosi vya Israel tarehe 23 Machi.

Daktari mmoja pekee wa PRCS alinusurika katika shambulio hilo na baadaye alieleza kuwa alitekwa na kuzuiliwa na vikosi vya Israel kwa takribani saa 15 kabla ya kuachiliwa.

Shirika la PRCS limetaja tukio hilo kama “uhalifu wa kivita”, likiituhumu Israel kwa mfululizo wa mashambulizi yaliyolengwa dhidi ya wafanyakazi wa afya na magari ya wagonjwa walipokuwa wakijibu wito wa kutoa msaada kwa waliojeruhiwa.

PRCS linasisitiza haja ya kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu tukio hilo, na kuchukuliwa hatua za kuwawajibisha waliohusika.

“Tunaomba jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na kuishinikiza Israel kumuachilia mara moja mwenzetu, daktari Assad, ambaye alitekwa akiwa anatekeleza wajibu wake wa kibinadamu.” Msemaji wa PRCS ameieleza New York Times

Jeshi la Israel, katika taarifa yake ya awali iliyotolewa Jumatatu iliyopita, lilisema uchunguzi wa ndani ulionesha wanajeshi walifyatua risasi wakidhani ni tishio, kufuatia tukio jingine katika eneo hilo, na kwamba watu sita waliouawa walihusishwa na kundi la Hamas.

Hata hivyo, halikutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.

Bw. al-Nassasra amehudumu ndani ya shirika hilo kwa zaidi ya miaka 16, na ni baba wa watoto sita.

Jeshi la Israel lilianzisha kampeni dhidi ya Hamas kufuatia shambulio la kuvuka mpaka la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu takriban 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 kutekwa nyara.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, zaidi ya watu 50,940 wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu kampeni hiyo ianze.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI