Header Ads Widget

BAKWATA SONGWE KUFANYA DUA MAALUM KUMUOMBEA RAIS, TAIFA NA UCHAGUZI MKUU.

 


Na Moses Ng'wat, Tunduma.

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Songwe limetangaza kuandaa dua maalum ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Taifa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.


Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Aprili 28, 2025, mjini Tunduma, Wilayani Momba,  Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Hussein Batuza, amesema dua hiyo mbali na kumuombea Rais, pia  inalenga kuombea Taifa na uchaguzi mkuu ili ufanyike kwa amani, haki na utulivu, huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo kwa wananchi wote.


"Dua hii ni maalum kwa ajili ya kumwombea Rais wetu, nchi yetu, na uchaguzi, ikiwemo kuwajenga wananchi kuwa wazalendo na kulinda amani yetu, hasa kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi" amesema Shekhe Batuza.


Kwa mujibu wa Shekhe Batuza, dua hiyo imepangwa kufanyika tarehe 17 Mei 2025 katika Shule ya Sekondari ya Vwawa, Wilayani Mbozi. 


Amesema, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo itakayowakutanisha waumini wa madhehebu yote ya dini, viongozi wa serikali, madiwani pamoja na wananchi wa kada mbalimbali.


Aidha, katika hatua nyingine Shekhe Batuza ametoa wito kwa wanasiasa na vyama vyao kuhakikisha wanazingatia taratibu zilizowekwa na Katiba, kuhubiri siasa safi bila matusi wala uchochezi, na kuhimiza matamko yanayojenga mshikamano wa kitaifa.


"Lazima tukemee kauli zote hatarishi na kushikilia tunu ya amani tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu," amesisitiza  Shekhe Batuza.



Naye, Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Songwe, Annuar Khan, amesema kuwa maandalizi ya dua hiyo yanaendelea vizuri huku juhudi zikiendelea za kuhakikisha madhehebu yote yanashiriki kwa pamoja katika kumuombea Rais kuelekea uchaguzi mkuu, pamoja na Taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA), Tutu Shilla, aliwahimiza wanawake wa Kiislamu kushiriki kikamilifu katika dua hiyo.


Amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha vijana kuepuka kushiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani, na kuendelea kuwasihi kupitia ibada misikitini na hata makanisani.


"Sisi kama walezi wa familia tuna jukumu la kuhakikisha vijana wetu wanabaki kuwa mabalozi wa amani. Tutashirikiana na viongozi wa dini zote kuhimiza upendo, mshikamano na utulivu kuelekea uchaguzi," amesema Shilla.


Kwa pamoja, viongozi wa BAKWATA Mkoa wa Songwe wametoa wito kwa wananchi wote kushiriki dua hiyo kwa wingi na kuwa sehemu ya juhudi za kulinda amani ya taifa, kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI