Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wamiliki na waendeshaji wa maboti ya uvuvi na usafirishaji kwa kutumia katika ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wameiomba serikali kuimarisha mawasiliano ya simu kwenye maeneo yote ya mwambao wa ziwa hilo ili kusaidia kutoa taarifa ya uokozi inapotokea ajali.
Wamiliki hao wametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa pamoja na viongozi na watendaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) uliokuwa na lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wamiliki wa maboti katika ziwa Tanganyika mkoani Kigoma sambamba na kuimhimiza utii wa sheria wamiliki hao wanapofanya kazi zao.
Mmoja wa wamiliki hao, Mussa Hamisi alisema kuwa wamekuwa wakipata hasara inapotokea dhoruba ziwani kwa kushindwa kupata mawasiliano ya watu waliopo kwenye boti ziwani ambapo kama mawasiliano yangepatikana ingeweza kuwa rahisi kuwaokoa.
Naye Kashindi Adamu alisema kuwa ni lazima serikali iliangalie suala hilo kwa makini kwani kwa sasa hakuna kituo cha uokoaji ziwa Tanganyika hivyo kuwepo kwa mawasiliano ya simu inaweza kusaidia kukabili tatizo linapotokea na kuomba serikali kuimarisha minara ya mawasiliano eneo kubwa la mwambao wa ziwa Tanganyika.
Akijibu hoja hizo za wamiliki, Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) makao makuu, Adam Mamilo alisema kuwa kwa sasa hakuna kituo cha uokoaji mkoani Kigoma na kwamba shirika hilo lina mpango wa kujenga kituo cha uokoaji katika ziwa Tanganyika kama ilivyo kwenye maziwa mengine nchini ili kusaidia ajali inapotokea na kwamba mchakato wa mradi huo umeshaanza.
Akizungumzia suala la ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye ziwa Tanganyika alisema kuwa ujenzi huo wa minara utaenda sambamba na ujenzi wa kituo cha uokoaji pindi mradi utakapoanza kutekelezwa ambapo pamoja na hilo amewataka wamiliki wa maboti na mabaharia kufuata sheria na taratibu zinazoongoza vyombo vya majini ili kuzuia ajali.
0 Comments