Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wananchi wa kijiji cha Kigogwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wameiomba serikali kuwasaidia kwa kuwapatia misaada ya hali na mali kutokana na kuathiriwa na mvua ya upepo ambapo nyumba zao zimebomoka na vitu vyao vya ndani kuharibika.
Wananchi hao wametoa kauli hiyo mbele ya Mbunge wa jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru aliyetembelea kijiji hicho kuwapa pole na kuwashika mkono kufuatia mvua za upepo baada ya paa za nyumba zao kuezuliwa na upepo na nyingine kuta kuanguka.
Mmoja wa waathirika wa mvua hiyo, Stephano Ezekiel alisema kuwa ameathirika kwa kiasi kikubwa baada ya nyumba yake kuezuliwa paa na kuta kuanguka akiwa ndani na mvua ikinyesha lakini Mungu amemsaidia kutoka salama ambapo ameathirika kutokuwa na makazi na vitu vyake vya ndani vyote vimeharibika.
Mwananchi mwingine wa kijiji hicho, Richard Maliseli alisema kuwa kwa sasa anaishi kwa mdogo wake kwani nyumba yake imeanguka hivyo tangu wiki iliyopita ambapo kadhia hiyo imetokea hajapata msaada wowote na kueleza kuwa wanafarijika mbunge kuwatembelea na kuwashika mkono kwa kidogo alichojaaliwa kuwaletea.
Akitoa taarifa ya maafa hayo Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kigogwe wilayani Buhigwe, Methusela Ntahonsigaye alisema kuwa jumla ya watu 25 wameathiriwa na mvua hiyo kwa nyumba zao kuezuliwa paa, nyingine kuanguka lakini pia baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kujeruhiwa na kwamba tayari kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji ilifanya tathmini na kupeleka taarifa kwa Mkuu wa wilaya Buhigwe na Mbunge kuona hatua za kuchukua katika kuwasaidia wahanga hao.
Mbunge wa jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma,Felix Kavejuru alifika kijijini hapo kuwapa mkono wa pole wananchi hao mwishoni mwa wiki iliyopita na kueleza kuwa ameguswa na kadhia iliyowapa hivyo kusaidia kidogo alichonacho ili kuwapa faraja wahanga hao.
Akiwa kijijini hapo Mbunge huyo wa jimbo la Buhigwe alitoa mkono wa pole kwa kukabidhi kiasi cha shilingi 50,000 kwa kila kaya iliyoathiriwa na mvua hiyo akiahidi pia kutoa bandari za bati kwa ofisi ya CCM tawi la Kigogwe na kanisa la Sabato ambayo yaliezuliwa paa zake.
Mwisho.
0 Comments