Na Hamida Ramadhan , Matukio Daima App Dodoma
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa imeeleza kushangazwa na ukimya wa Baraza la Wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) kuhusu shambulio lililomkabili Mwenezi wa BAWACHA Taifa, Sigrada Mligo, mwenye umri wa miaka 34.
Tukio hilo lililotokea Machi 25, 2025, mjini Njombe, lilihusisha shambulio la mwili linalodaiwa kufanywa na mmoja wa walinzi wa chama hicho wakati wa kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche.
Shambulio hilo lilileta hofu miongoni mwa wanachama wa BAWACHA na kusababisha maswali mengi kuhusu usalama wa viongozi wa kisiasa nchini.
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, amelaani shambulio hilo na kuitaka Polisi Mkoa wa Njombe kuendeleza juhudi za kumsaka mtuhumiwa ili akabiliwe na sheria.
"Hatuwezi kuvumilia vitendo vya ukatili katika siasa. Ni lazima kila kiongozi ajisikie salama katika mazingira ya kazi yake," alisema Chatanda.
Aidha, UWT imesisitiza umuhimu wa kutoa elimu juu ya haki za wanawake na usalama katika siasa, akiongeza kuwa ni wakati muafaka kwa vyama vyote vya siasa kuungana kupinga ukatili wa aina yoyote dhidi ya viongozi wanawake.
Ujumbe wa UWT unasisitiza kuwa, kukosekana kwa kauli kutoka BAWACHA kunadhihirisha hali ya kutokubaliana na vitendo vya unyanyasaji, ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa dhati na kwa haraka.
Mwisho.
0 Comments