Header Ads Widget

NBC BANK YAZINDUA NBC SHAMBANI KUMWINUA MKULIMA MBEYA NA SONGWE.

 


Na Matukio daima App.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), imetambulisha kampeni yake ya ‘Wekeza NBC shambani ushinde’ kwa wakulima wa mazao mballimbali ikiwemo Kahawa na ufuta kwenye mikoa ya Songwe na Mbeya ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia uchumi jumuishi unaochagizwa na huduma rasmi za kifedha.


Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika katika kata ya Mlowo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, ikiongozwa na Katibu Tawala Wilaya ya Mbozi Mbwana Kambangwa, huku pia ikihusisha uwepo wa wadau mbalimbali wa sekta za kilimo na ufugaji kutoka mikoa hiyo miwili wakiwemo viongozi wa vyama vya msingi  na vyama vikuu vya ushirika vya wakulima na wafugaji (AMCOS) na wadau wengine wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hiyo muhimu.


Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa amewaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo inayotoa fursa kwa wakulima na wafugaji wa mikoa ya Songwe na Mbeya kushinda zawadi mbalimbali ikiwemo pikipiki na kompyuta mpakato ‘Laptops’ huku wakifaidika kwenye sekta hiyo.


Akizungumza kwenye hafla hiyo pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa jitihada zake endelevu zinazolenga kuwasaidia wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini ukiwemo mkoa wa Songwe, Kambangwa amesema ujio wa kampeni hiyo kwenye mikoa hiyo utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa wadau mbalimbali wa sekta hizo hususani kupitia huduma mbalimbali za kibenki zilizobuniwa mahususi kwa makundi hayo ikiwemo elimu ya kifedha na huduma za mikopo rafiki.


“Ubora zaidi wa kampeni hii unaonekana pale inapohusisha utoaji wa elimu ya nidhamu ya fedha miongoni mwa wakulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika hatua ambayo itawajengea uwezo wa kuona umuhimu wa kujiwekea akiba, umuhimu wa kutumia bima mbalimbali ikiwemo bima ya afya, bima za kilimo pamoja na kuwekeza kwenye zana za kisasa za kilimo’’, amesema na kuongeza.


“Hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha wakulima wetu kugeukia huduma rasmi za kifedha na hivyo kuchochea uchumi jumuishi. Hii ni hatua kubwa sana ikilinganishwa na tulipotoka miaka kadhaa iliyopita ambapo wakulima na wafugaji walikuwa hawaaminiki na taasisi za kifedha kutokana na kutokuwa waaminifu na wengine kutokuwa na dhamana", ameongeza.


Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo inayotarajiwa kuhitimishwa juni 15, 2025, Urassa amesema walengwa wa kampeni hiyo ni wakulima wa mazao mbalimbali hususani Kahawa na Ufuta kupitia  vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika na mkulima mmoja mmoja ambao wanahudumiwa na benki hiyo.


Kwa mujibu wa Urassa, ili mkulima mmoja mmoja ashinde zawadi ya pikipiki anatakiwa kwenye akaunti yake awe na fedha kiasi kisichopungua Million tano na kwa upande wa AMCOS na vyama vikuu vya ushirika zinatakiwa kuhifadhi kwenye akaunti zao za NBC Shambani  fedha kuanzia kiasi cha Sh. Mil. 5 hadi Mil. 50 ili kujishindia laptop na kuwa na fedha kwenye akaunti zao kiasi kisichopungua Sh. Mil 50 ili kujishindia pikipiki.


“Lengo la kampeni hii ni kuwahamasisha wakulima na wafugaji kutunza fedha zao kwenye mifumo rasmi ya kifedha hasa benki badala ya kutunza kwenye mifumo isiyo rasmi. Tunawakaribisha sana kufungua akaunti zao za NBC Shambani ili wawe kwenye nafasi ya kushinda zawadi hizi’’ amesema.


Akizungumza kwa niaba ya wakulima hao, Makamu Mwenyeki wa AMCOS ya Mwanjelwa, iliyopo wilayani Mbozi, Imani Luvanda amesema kwa kiasi kikubwa wakulima wilayani humo wamekuwa wakiumizwa na gharama za makato ya uendeshaji wa akaunti zao za benki pamoja na kufungwa kwa akaunti zao pindi zisipotumika kwa muda  kitu ambacho kimekuwa kikisababisha wengi wao kupoteza imani na matumizi ya taasisi rasmi za kifedha.


“Ila sasa kilichotuvutia zaidi kwenye akaunti hii ya NBC Shambani ni kwamba haina makato yoyote ndio kwanza mkulima anapata faida na zaidi haifungwi kiurahisi hadi ipite miaka miwili. Hii kwetu ni habari njema na binafsi takuwa balozi wa kuwaelimisha wenzangu kuhusu kampeni hii na faida za akaunti ya NBC Shambani’’, amesema makamu mwenyekiti huyo.


Mwisho 












Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI