Na Philipo Hassan - Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa Wizara imeweza kudhibiti shughuli za ujangili katika maeneo yaliyohifadhiwa na kupelekea ongezeko la idadi ya wanyamapori ikiwemo Tembo, Simba, Chui na Nyati.
Balozi Dkt. Chana ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani, yaliyofanyika katika Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma leo Machi 03, 2025 ambapo alipongeza taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kusimamia maeneo yaliyo hifadhiwa na kupambana na ujangili.
“Nchi yetu inaongoza kwa idadi kubwa ya wanyamapori, tunayo idadi kubwa ya Simba, Chui, Nyati na niseme kwamba Tanzania ni ya tatu (3) kwa kuwa na idadi kubwa ya Tembo Duniani” aliongeza Balozi Dkt. Chana.
Naye, Mkurugenzi wa Wanyamapori Tanzania, Dkt. Allex Lobora alieleza umuhimu wa kuadhimisha siku hiyo ambapo inaikumbusha jamii kulinda na kuhifadhi maliasili zetu ikiwemo wanyamapori na mimea iliyopo hatarini kutoweka, kupunguza uharibifu wa mazingira na kuzuia ujangili.
Dkt. Lobora aliongeza “ Siku hii inatoa fursa ya kuonyesha mchango wa wanyamapori katika maisha ya binadamu pamoja na kuhamasisha hatua za kulinda wanyamapori kwa manufaa ya vizazi vijavyo”
Aidha, kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema “Wanyamapori na Uwekezaji Kifedha, Wekeza kwa Watu na Dunia” huku ikihimiza kuwa na mifumo na mikakati endelevu ya kupata na kusimamia matumizi ya rasilimali ili kufikia lengo la uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano ya amani kutoka Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii Swagaswaga kuelekea Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma ambapo Balozi Dkt. Chana alitembelea mabanda yaliyokuwa yakitoa taarifa kuhusu elimu uhifadhi na utalii.
0 Comments