Na Moses Ng’wat, Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amekutana na ujumbe kutoka Benki ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Ujerumani (KfW) pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Maji kujadili uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji safi na salama katika wilaya za Momba na Mbozi.
Katika kikao kilichofanyika, Machi 3, 2025, Chongolo aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania, hasa katika sekta ya maji.
Alieleza kuwa mpango huo unalenga kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ambapo huduma hiyo ipo chini ya asilimia 50.
"Awali, tulikuwa tunajiuliza kuhusu gharama kubwa za kupeleka maji katika maeneo hayo hasa kwa kutumia chanzo kimoja cha mto uliopo kilomita 48 kutoka hapa, lakini sasa tuna uhakika kuwa uwekezaji huu wa KfW utatoa matokeo sahihi na naamini mwelekeo huu utakuwa na tija zaidi kwetu." Alisisituza Chongolo.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Nicodemus Angumbwike kutoka Wizara ya Maji alifafanua kuwa KfW imekuwa mdau muhimu katika kufadhili miradi ya maendeleo nchini, hususan katika sekta ya maji.
Alisema benki hiyo ina mpango wa kuwekeza Euro milioni 20 (ambayo ni sawa na shilingi bilioni 50) ili kutekeleza mradi wa maji katika miji ya Tunduma, Vwawa, na Mlowo.
Aidha, Simone Sieler, Meneja Mwandamizi wa Hazina ya Miradi, Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika kutoka KfW, aliishukuru Wizara ya Maji na serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake na Serikali ya Ujerumani.
Alibainisha kuwa uwekezaji huu unatarajiwa kusaidia kupunguza uhaba wa maji na kuboresha maisha ya wakazi wa wilaya za Momba na Mbozi.
Mwisho.
0 Comments