Header Ads Widget

TUNZENI VYANZO VYA MAJI-MAUWASA.

WAJUMBE wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa na watumishi wa Mauwasa wakiangalia jinsi mtambo wa kutibu na kusafisha maji unavyofanya kazi ulioko katika kijiji cha Zanzui.


Na Samwel Mwanga, Maswa.


WANANCHI wa wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, wametakiwa kuacha shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kuzunguka vyanzo vya maji hatua ambayo itawezesha upatikanaji  wa maji ya kutosha na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.


Hayo yameelezwa leo, Machi 22, 2025, wakati wa kilele cha wiki ya maji na Leonard Mnyeti ambaye alikuwa akimwakilisha  Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) wakati akizungumza na Wajumbe wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa, waliotembelea katika chanzo cha maji cha Bwawa la New Sola katika kijiji cha Zanzui.


Amesema wengine wamekuwa wakiingiza mifugo jambo ambalo hawawezi kulifumbia macho na amewataka viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji na vijiji kusimamia ulinzi wa vyanzo hivyo na kudhibiti  uharibifu.


Amesema kuwa bwawa hilo ambalo ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji wa Maswa na vijiji 19 linalotegemewa na zaidi wa watu 102,682 limepunguza kina cha maji kutokana na kuingiza tope.


“Tumetembelea chanzo chetu cha maji ambacho ni bwawa la New Sola lina lita za ujazo Milioni 4.2 na chanzo chake kikubwa ni mto Sola ila kutokana na shughuli za kibinadamu kufanyika kandokando ya mto huo kina cha maji kimepungua kwa sasa na kuwa na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 4 tu,” Amesema na kuongeza.


“Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake kuhakikisha vyanzo hivi vinatunzwa ili viweze kuwa endelevu,”.


Caroline Shayo ni mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa, amesema kuwa ni vizuri  wananchi kujenga utamaduni wa kupanda miti rafiki kwa mazingira kuzunguka vyanzo vya maji na hata kwenye nyumba zao ili kukabiliana na athari za ukame.


“Niwatake viongozi wenzangu kila mmoja katika eneo la  kuhubiri utunzaji wa vyanzo vya maji, wananchi wetu tuwaelimishe kupanda miti rafiki ya mazingira na vizuri tunze na sisi pia tuwachukulie hatua wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji,” amesema.


Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwabomba, Masanja Mshandete amesema kuwa mamlaka hiyo iendelee na juhudi za kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira hasa kwa wakulima na wafugaji hasa katika ulinzi wa bwawa hilo.


“MAUWASA iendelee kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji,tunatambua kuwa katika jamii zetu kuna kundi la wakulima na wafugaji lakini kwa pamoja tuna jukumu la kuvilinda vyanzo vyetu vya maji huku shughuli za kilimo na ufugaji zikiendelea kwa kufuata utaratibu uliowekwa,” amesema.


John Gogadi ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Majebele wilayani humo, amesema kuwa serikali inatambua na kuthamini ufugaji mzuri unaozingatia kutoharibu mazingira  hasa kwenye vyanzo vya maji.


“Hili halikubaliki,fuga kulingana na uwezo wa eneo lako la malisho,tunawapenda wafugaji lakini ni lazima wafuate utaratibu kwa kutoingiza mifugo yao katika vyanzo vya maji,” amesema.


MWISHO. 


Sehemu ya chujio la kutibu na kuchuja maji katika chanzo cha maji katika bwawa la New Sola wilayani Maswa.


Kaimu Mkurugenzi mtendaji MAUWASA, Leonard Mnyeti akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kilele cha wiki ya maji 2025.


Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa, Caroline Shayo akizungumza baada ya kutembelea chanzo cha maji cha Bwawa la New Sola.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI