Header Ads Widget

TAKUKURU SINGIDA YAWATAKA WANAWAKE KUPINGA RUSHWA YA NGONO

 



Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imewataka wanawake kujitambua na kukataa rushwa ya ngono ili wapandishwe vyeo, kuchaguliwa au kuteuliwa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa kuwa vitendo hivyo vinadhalilisha utu wao.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala, alisema hayo jana wakati wa bonanza la michezo lililofanyika uwanja wa Bombadia Manispaa ya Singida ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho kuelekea Siku ya Wanawake Duniani ambayo yatahitimishwa Machi 8, 2025.

Alisema rushwa ya ngono imekuwa changamoto sana kwa wanawake mfamo wanawake wajasiriamali wamekuwa wakiombwa rushwa hiyo ili wapate leseni na kwa wanawake ambao ni watumishi wa serikali wanaombwa rushwa ya ngono ili waweze kupandishwa cheo au kupewe safari zenye posho.





"Wanawake kwa sasa waamke wajitambue wakatae kutoa rushwa ya ngono kwani rushwa ni mbaya na adui wa haki inadhalilisha utu wa mwanamke, kwa hiyo tunawaomba wanawake wasaidie kufichua vitendo hivyo ili TAKUKURU iweze kuchukua hatua za kuchunguza na kuwafikisha wahusika mahakamani, "alisema

Mwanjala alisema ili wanawake waweze kuwezeshwa ni lazima wakatae rushwa ya ngono na ndipo wataweza kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu ambao ni haki yao ya msingi kushiriki na kuweza kuchaguliwa.

"Rushwa haiwezi kuisha endapo tutazidi kunyamazia vitendo hivi tena tena tukiwa watekelezaji wake, wanawake chukueni hatua madhubuti ya kukataa vitendo hivi vya rushwa ya ngono," alisema.

Aidha,Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Singida alitumia bonanza hilo kutoa elimu kwa wanawake juu ya madhala ya rushwa ya ngono inavyonyanya wanawake na kuzorotesha maendeleo.

Kwa upande wake Jenny Hamis na Mariam Juma ambao walipata elimu hiyo waliishukru TAKUKURU kwa kuwapa elimu ambayo imewafanya watambue madhala ya rushwa ya ngono.

Mwaka jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene,i aliwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024, ambao ulipendekeza kuongeza adhabu ya faini isiyopungua Shilingi milioni mbili na isiyozidi Sh. milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka mitano kwenye makosa ya rushwa ya ngono.

MWISHO


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI