Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
MAADHIMISHO ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Machi 8, maandalizi yamekamilika katika Mkoa wa Singida ambapo miongoni mwa mambo yatakayofanyika ni pamoja na kongamano ambalo litawajumuisha takribani wanawake 1,000 kutoka ngazi ya vijiji hadi mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akizungumza na waandishi wa habari leo (Machi 1, 2025) amesema maandalizi yamekamilika na leo Machi 1, 2025 yameanza kufanyika katika ngazi za chini yaani kitongoji, kijiji, kata,tarafa na halmashauri ambapo yataendelea kuazimishwa katika ngazi hizo hadi Machi 4, 2025.
Amesema itakapofika Machi 5, maadhimisho yataanza katika ngazi ya mkoa na maandalizi yake yameshakamilika ambapo mambo yatakayofanyika ni kwa viongozi kuwatembelea watu wenye mahitaji maalum ikiwa ni maelekezo mahususi ya maadhimisho ya mwaka huu.
"Tutawatemebelea watu wenye mahitaji maalum katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Singida kuwaona vijana wetu wenye ulemavu kuwapa faraja kwa kuwapatia zawadi mbalimbali, kucheza nao na kwa wale ambao hawatakuwa kwenye mwezi mtukufu watakula nao chakula pamoja," amesema Dendego.
Mkuu wa Mkoa amesema siku hiyo hiyo kutakuwa na bonanza kubwa la michezo kwenye viwanja vya Bombadia Manispaa ya Singida ikihusisha mchezo wa mpira wa miguu,mpira wa mikono,ngoma za utamaduni na mziki wa kizazi kipya.
Ameongeza kuwa Machi 6, 2025 kutakuwa na kongamano litakalowajumuisha wanawake takribani 1000 kutoka maeneo mbalimbali kuanzia ngazi za vijiji hadi mkoa ambao watafundisha mada mbalimbali ikiwamo wap wenyewe kujitambua na kuielewa historia ya wanawake duniani,nishati safi ya kupikia na mwanamke na uchumi.
Mada nyingine watakazofundishwa wanawake ni mwanamke na kodi,masuala ya ukatili wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika kuhakikisha anakuwa mama bora na wanatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kaya.
Aidha,amesema Mkoa wa Singida utayatumia maadhimisho hayo kwa kugawa mitungi ya gesi 29,000 yenye bei ya ruzuku kwa wanawake ikiwa ni hatua kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mkoani hapa.
"Rais Dk.Samia Suluhu Hassan yeye ndiye kinara wa nishati safi duniani kwa hiyo katika taifa lake ameweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunawafikia watu wengi kwa nishati safi ya kupikia na serikali inakuwa ndio namba moja na wadau wengine wanafuata," amesema Dendego.
Amesema katika mpango huo wa kuhamaisha matumizi ya nishati safi ya kupikia serikali imekuja na ruzuku ya mitungi ya gesi ambayo inauzwa kwa nusu bei na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ndio wamepewa dhamana ya kusambaza majiko na mitungi ya gesi nchini.
MWISHO
0 Comments