Header Ads Widget

PIC: MIRADI WA MAJI KIGOMA UJIJI UTAONDOA KERO KWA WANANCHI

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji  Mitaji ya Umma (PIC) imesema kuwa miradi ya maji inayotekelezwa kwa gharama kubwa lazima ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi katika kutimiza azma ya serikali ya kumtua mama ndoo kwa kuhakikisha huduma zinapatikana karibu na wanapoishi watu.

Mwenyekiti wa Kamati ya PIC ,  Augustino Holle Vuma alisema hayo akihitimisha ziara ya kamati hiyo ilipofanya ziara kutembelea na kukagua mradi mkubwa wa maji katika manispaa ya Kigoma Ujiji unaotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira  Kigoma (KUWASA).

Mbunge huyo  alisema kuwa serikali imewekeza kiasi kikubwa cha pesa kwenye mradi huo kwa ajili ya kutatua kero ya upatikanaji wa maji safi na salama hivyo miradi hiyo lazima ilete tija kwa kuondoa kero kwa wananchi.

Pamoja na hilo Vuma ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kuwezesha kukamilika kwa mradi huo kutoka chanzo cha  Aman Beach sambamba na kuipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) kwa kusimamia mradi huo na kwamba kamati imeridhika na utekelezaji wa mradi huo  ambapo imeitaka mamlaka hiyo kuhakikisha inaongeza mtandao wa usambazaji wa maji ili kuwafikia wananchi wengi Zaidi.

Akitoa taarifa kwa kamati ya bunge ya PIC Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Poas Kilangi, alisema kuwa mradi huo ulioanza mwaka 2013 umegharimu kiasi cha shilini Bilioni 42 ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 kwa siku ukilenga kuwahudumia wateja 25,309 ambapo kwa sasa unatoa huduma kwa asilimia 92.

Kilangi alisema kuwa pamoja na kukamilika kwa mradi huo na kuanza kutoa huduma pia mamlaka hiyo inaendelea na jitihada za kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kusaini mikataba ya ujenzi wa vituo vya kusukuma maji katika maeneo ya Mwasenga na Masanga pamoja na vijiji vya Kasaka, Kazegunga, na Msimba na kwamba kutanua mtandao wa maji na kuboresha huduma  kwa kilometa 406 kutawezesha mradi kutoa huduma kufikia asilimia 95 kufikia mwezi Desemba mwaka huu.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI